Chelsea VS Liver moto

Muktasari:

Timu yoyote itakayoshinda basi itaifanya Englannd kushinda taji lake la nane la Uefa Super Cup, ikiwa imezidiwa na Hispania mara 15 na Italia mara tisa.

Istanbul, Uturuki . MOTO unawashwa Ulaya wakati Liverpool itakapokipiga na Chelsea kwenye mechi kali ya Uefa Super Cup kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Besiktas Park, Istanbul, Uturuki.

Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa timu mbili za Uingereza kukutana kwenye mechi hiyo hasa baada ya Liverpool kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Chelsea kunyakua Europa League msimu uliopita.

Huo ni mtihani mwingine mgumu kwa Kocha Frank Lampard, ambaye juzi Jumapili alishuhudia kikosi chake kikichapwa mabao 4-0 na Manchester United katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England.

Liverpool ikiwa chini ya Kocha Jurgen Klopp, yenyewe itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu tamu ya ushindi wa mabao 4-1 katika mechi yao iliyopita ilipoichapa Norwich City kwenye Ligi Kuu.

Timu yoyote itakayoshinda basi itaifanya Englannd kushinda taji lake la nane la Uefa Super Cup, ikiwa imezidiwa na Hispania mara 15 na Italia mara tisa.

Kwa England timu ya mwisho kubeba taji hilo ilikuwa Liverpool mwaka 2005. Chelsea yenyewe ilichapwa 2012 na 2013.

Fainali saba za Uefa Super Cup zilizopita zimehusisha timu za kutoka ligi moja, mbili za Italia, tano za Hispania zikiwamo nne kuanzia mwaka 2014, huku ya karibuni ni ile Atletico Madrid ilipoichapa Real Madrid mwaka jana. Lakini kwa Chelsea na Liverpool hii ni mara yao ya 11 kukutana kwenye michuano ya Uefa kwa kuanzia mwaka 2005, ambapo mechi 10 zilikuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo tano zilimalizika kwa sare, mbili ikishinda Liverpool na tatu Chelsea, huku mechi moja tu ndiyo iliyoshuhudia tofauti ya zaidi ya bao moja.

Katika mechi zao zote za michuano tofauti, Liverpool na Chelsea zimekutana mara 181, Liverpool ikishinda 77, Chelsea 63 huku kukiwa na sare 41.

Lakini mechi hiyo ya kesho imekuwa na rekodi tofauti kabisa huku ikimfanya Lampard kuwa kwenye mtihani mzito wa kukwepa kipigo cha pili mfululizo baada ya kupewa mikoba ya kuinoa timu hiyo ya Stamford Bridge. Alipokuwa mchezaji, Lampard aliifunga Liverpool mabao saba katika mechi 39, huku akiwa na rekodi ya ushindi mara 18, sare nane na kupoteza 13 katika mechi alizokabiliana na Liverpool.

Mechi hiyo itamshuhudia pia staa Mohamed Salah akichuana na waajiri wake wa zamani ambao ndio hasa waliokuwa wa kwanza kumwonjesha soka la England, wakati ilipomnasa kutoka FC Basel Januari 2014. Salah aliichezea Chelsea mechi 19 tu, akifunga mabao mawili, kabla ya kwenda Fiorentina, kisha AS Roma na sasa Liverpool.

Fainali hiyo itakutanisha pia wachezaji kadhaa waliowahi kucheza timu moja huko nyuma, lakini kwa hiyo kesho watakuwa wapinzani, akiwamo Salah na Emerson na Antonio Rudiger waliowahi kucheza pamoja AS Roma. Alisson Becker, Emerson na Rudiger nao walicheza pamoja Roma, huku Salah na Marcos Alonso walikuwa pamoja Fiorentina na Fabinho na Tiemoue Bakayoko walikuwa pamoja AS Monaco.

Fainali hiyo ya Uefa Super Cup ni bato la wakali wanaofahamiana vyema kutokana na kuwapo pia mastaa kibao wanaochezea timu moja za taifa kama vile Dejan Lovren na Mateo Kovacic huko Croatia, Alisson na Willian Brazil, Ross Barkley na Jordan Henderson England kwa kuwataja kwa uchache tu.