Chelsea, United kumaliza utata

Muktasari:

  • Ubora wa mechi wa Chelsea na Man United unategemea na Eden Hazard na Paul Pogba kila upande. wanapokuwa bora timu zao zinakuwa bora, wanapochemka na timu pia zinachemka.

LONDONENGLAND . CHELSEA na Manchester United ndio kama ulivyosikia. Makocha wawili, Maurizio Sarri na Ole Gunnar Solskjaer wameonyeshana ubabe kwenye mchezo wa raundi ya tano ya Kombe la FA, huku kila mmoja akipambana kulinda kibarua chake.

Timu hizo mbili kwa pamoja zimebeba Kombe la FA mara 20, Man United ikinyakua mara 12 na Chelsea mara nane. Arsenal ndio inayoongoza kihistoria, imebeba taji hilo mara 13.

Rekodi zilikuwa zikimbeba Sarri kwa mchezo huo uliopigwa na jana Jumatatu usiku huko Stamford Bridge. Ushindi wowote wa Chelsea usingeshangaza kutokana na rekodi zake za hivi karibuni ilipocheza na Man United kwenye michuano hiyo.

Ubora wa mechi wa Chelsea na Man United unategemea na Eden Hazard na Paul Pogba kila upande. wanapokuwa bora timu zao zinakuwa bora, wanapochemka na timu pia zinachemka.

Kabla ya mechi ya jana, Chelsea na Man United zilikutana mara mbili kwenye michuano hiyo hivi karibuni na mechi zote hizo, The Blues ilishinda Moja Bila. Hiyo ni pamoja na fainali ya mwaka jana, Eden Hazard alifunga na ile ya robo fainali, N’Golo Kante alifunga.

Lakini kipindi Man United anakumbana na mateso hayo, makocha walikuwa wengine. Chelsea ilikuwa Antonio Conte na huko Man United alikuwa Jose Mourinho. Mechi hiyo ya usiku wa jana ilikuwa vita ya Sarri na Solskjaer. Shida ilikuwa rekodi za Man United kwenye mechi zake dhidi ya Chelsea kwenye michuano hiyo. Mara ya mwisho Man United kuishinda Chelsea kwenye Kombe la FA ilikuwa mwaka 1999. Si kama hapo kati mechi hazikuchezwa, zilichezwa na ushindi wa Man United katika muda wa kawaida ulikuwa sare tu, mechi nyingine zote amechapwa. Ukiacha mechi mbili za karibuni, kutoka 1999, zilichezwa mechi tano, Chelsea imeshinda mbili na nyingine tatu zilizomalizika kwa sare, huku The Blues ikisonga mbele kwa sababu mechi hizo zote zilikuwa za kutoana. Solskjaer alikuwa na shughuli pevu kubadili hali hiyo na kuirudisha United kwenye zama za kuitesa Chelsea kwani kutoka mwaka 1999 kurudi nyuma, Man United iliitesa sana The Blues kuna mechi moja ya raundi ya tatu kwenye Kombe la FA, Chelsea ilichapwa Bao Tano kwenye matoke ya 5-3, Januari 1998.