Cheki pesa iliposhindwa kununua mapenzi kwa mastaa hawa

Muktasari:

Kuna wanasoka wamekuwa na mapenzi makubwa sana kwa baadhi ya timu kiasi kwamba hata wapewe ofa tamu kiasi gani na timu nyingine, kuamua kubali walipo au kwenda wanakotaka wao, haliwezi kuwa jambo la ajabu.

LONDON, ENGLAND. WANASEMA hivi, pesa haina uwezo wa kununua mapenzi ya dhati. Hilo lipo katika maisha ya kawaida na lipo pia kwenye maisha ya wanasoka. Kuna wanasoka wamekuwa na mapenzi makubwa sana kwa baadhi ya timu kiasi kwamba hata wapewe ofa tamu kiasi gani na timu nyingine, kuamua kubali walipo au kwenda wanakotaka wao, haliwezi kuwa jambo la ajabu.
Wanasoka hawa hapa walipata ofa tamu ya kwenda kujiunga na klabu vigogo vya Ulaya, lakini wakagoma na kufanya kile wao walichokiona kinafaa kwenye mapenzi yao juu ya mchezo huo. Mapenzi yao hayakununuliwa kwa pesa.

5.Gianluigi Buffon – Barcelona
Mmoja wa makipa bora kabisa duniani ambao hawahitaji utambulisho. Mwaka 2001, Buffon alipata ofa ya kutoka Barcelona kwamba akienda Nou Camp atapata namba moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza. Kipindi hicho Barca walikuwa vizuri na wengi waliamini kwamba kipa huyo Mtaliano asingechomoa kwenda kujiunga na timu hiyo, huku kukiwa na ripoti kwamba hata mshahara wake ungekuwa wa kibosi akitua huko Nou Camp. Lakini, Buffon alishangaza wengi baada ya kuamua kwenda kujiunga na Juventus. Kwa sasa anakipiga huko Paris Saint-Germain alikojiunga kwenye dirisha lililopita la usajili baada ya kuamua kuachana na wababe wa Italia, Juventus.

4.Diego Godin – Man City
Wakati Manchester City wakibeba ubingwa wa ligi England katika msimu wa 2013/14, huko Hispania nako kulitokea maajabu, wakati Atletico Madrid walishinda taji la La Liga. Kwenye kikosi cha Atletico kulikuwa na beki matata, Diego Godin na kwa wakati huo alikuwa akisakwa na vigogo wa Ulaya. Kocha wa Man City kwa wakati huo, Manuel Pellegrini alivutiwa na Godin kumtaka kwenye kikosi chake. Kwenye mpango huo, Pellegrini alikuwa tayari kulipa Euro 40 milioni kununua mkataba wa Godin kama ulivyoelezwa kwenye moja ya vipengele vya mkataba wake. Lakini, Godin aliamua kupuuzia nafasi ya kwenda kuvuna mshahara mkubwa huko Etihad na kubaki zake Atletico na kocha wake, Diego Simeone. Kwenye dirisha lililopita la usajili wa majira ya kiangazi huko Ulaya, Godin aligomea pia ofa ya kwenda kujiunga na Manchester United.

3.Steven Gerrard – Real Madrid
Mwaka 2004, Chelsea walifanya jaribio la kutaka kumsajili kiungo wa Liverpool, Steven Gerrard, ili akajiunge kwenye kikosi chao huko Stamford Bridge. Kila kitu kilionekana kuwa ni kweli baada ya ujumbe wa simu aliotuma Gerrard kwenda kwa kocha Jose Mourinho, aliyekuwa Chelsea kwa wakati huo kuvunja. Gerrard alimwaandikia Mourinho ujumbe huu: "Nataka kukwambia kwamba nipo tayari kujiunga na Chelsea.” Lakini, ghafla mambo yalibadilika na Gerrard akabaki Liverpool. Baadaye akiwa na Real Madrid, Mourinho alifanya mchakato mwingine wa kumnasa Gerrard na ilionekana kama Mwingereza huyo asingekataa ofa ya kutua Bernabeu, cha ajabu akabaki zake Anfield na kugomea ofa hiyo matata kabisa.

2.Xavi – Bayern Munich
Wakiwa wamebeba taji moja tu katika msimu wa 2013/14, ilielezwa huo ni mwaka mgumu zaidi katika historia ya Barcelona katika muongo mmoja kwa kubeba taji moja. Kipindi hicho, Bayern Munich ya Pep Guardiola ilikuwa matata kabisa huko Ujerumani. Kitu ambacho Bayern walikifanya ni kupeleka ofa ya kumnasa kiungo huyo fundi wa mpira, lakini ajabu Xavi aligomea ofa hiyo. Wengi waliamini kwamba Xavi angekubali kwenda kuungana na kocha wake wa zamani, Mhispaniola mwenzake, Guardiola huko Allianz Arena na akabaki zake La Blaugrana.

1.Jamie Vardy – Arsenal
Leicester City walithibitisha kwamba hakuna kisichowezekana wakati walipobeba ubingwa wa Ligi Kuu England katika msimu wa 2015/16. Kiwango bora cha straika Jamie Vardy kilichangia kwa kiasi kikubwa sana ubingwa huo. Msimu uliofuatia, Arsenal walihitaji huduma ya mshambuliaji huyo na kutaka kumsajili, wakimpa ofa ya mkataba mrefu aende akachukue mikoba ya Oliver Giroud. Lakini, cha ajabu Vardy hakutaka kwenda Arsenal na badala yake aliamua kubaki zake King Power kuendelea kuitumikia Leicester City.