Cheki kilichoibeba Tanzania tenisi Afrika

Muktasari:

Katika mechi za mkondo wa pili, Tanzania ilishinda medali nne za shaba kwa wasichana na wavulana chini ya miaka 16 na 14, ushindi ulioiweka katika nafasi ya tatu kwenye matokeo ya jumla, ikiongozwa na Rwanda na Kenya.

Tanzania imeingia kwenye orodha ya nchi tatu bora Afrika Mashariki na kati kwenye tenisi ya vijana chini ya umri wa miaka 16 na 14.

Matokeo hayo ni moja ya mafanikio kwenye mchezo huo nchini mwaka huu baada ya wachezaji Kanuti Alagwa, Rashid Ramadhan, Isaka Ndossi, Ismael Rashid, Naitoti Singo na Nasha Singo kutwaa medali kwenye mashindano ya mkondo wa pili Afrika Mashariki na Kati yaliyofungwa juzi jijini Dar es Salaam.

Awali, Kanuti alitwaa dhahabu kwenye mashindano ya mkondo wa awali ya vijana chini ya umri wa miaka 16 wakati Rashid akitwaa fedha kwenye umri chini ya miaka 14 na Naitoti alishinda shaba kwa wasichana.

Katika mechi za mkondo wa pili, Tanzania ilishinda medali nne za shaba kwa wasichana na wavulana chini ya miaka 16 na 14, ushindi ulioiweka katika nafasi ya tatu kwenye matokeo ya jumla, ikiongozwa na Rwanda na Kenya.

Mechi za mkondo wa pili zilitoa pointi kwa nchini zikishirikisha wachezaji wawili wawili katika kila umri ambao walicheza mechi za singles kisha kucheza double na walioshinda michezo yote mitatu au miwili wanaipa nchi yao pointi kabla ya Tanzania kuvuna medali za shaba katika makundi yote.

Ndossi na Rashid ndiyo waliofungua pazia la medali kwa Ndossi kumfunga Michael Gomme seti 2-0 za 6-3 na 6-2 na Rashid kumchapa Matteo Lavigne seti 2-0 za 6-3 na 6-2.

Kwa wasichana, Naitoti na Nasha ambao ni ndugu waliwafunga Paula Awino na Maggie Namaganda seti 2-0 kila mmoja za 6-2 na 6-4 na 7-6 na 6-3.

Kanuti na Ismael walitwaa shaba kwa kuwafunga Raymond Oduor na Edmond Ogega wa Kenya, wakati wasichana nao wakitwaa medali ya shaba huku Kenya ikitwaa ubingwa kwa kuichapa Uganda katika michezo miwili kati ya mitatu ya fainali.

Alicia Owegi amemfunga Shanita Namagembe kwa seti 2-0 za 6-0 na 6-0 wakati Angela Akutonyi akimchapa Winnie Birungi kwa seti 2-0 za 6-1 na 6-2.

Nyota Tanzania wafunguka

“Ilikuwa ni juhudi ya kila mmoja wetu, kuanzia makocha, viongozi na sisi wachezaji,” alisema Kanuti miongoni mwa nyota wa Tanzania anayechipukia.

Naitoti alisema licha ya malengo yao yalikuwa ni ubingwa, lakini uzoefu wa kimataifa ndiyo uliwanyima medali za dhahabu.

“Wenzetu hasa Rwanda ni wazoefu na mashindano ya kimataifa kulinganisha na sisi,” alisema mchezaji huyo wa kike ambaye mashindano hayo yalikuwa ya pili ya kimataifa kwake kushiriki.

Alisema kuna haja sasa nao wapewe fursa ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya ITF.

“Hii itatujengea kujiamini zaidi, mfano mimi, hii ni mara yangu ya pili kwenye mashindano ya kimatifa, lakini nimeshinda medali mbili za shaba, kama tukipata nafasi zaidi hatukosi dhahabu,” alisema.

Nyota wa Rwanda, Junior Hakizumwami anasema, Tanzania imebadirika hivi sasa kulinganisha na miaka ya nyuma.

“Kuanzia wachezaji, viwanja na hata maandalizi, mwaka huu yalikuwa vizuri,” alisema mchezaji huyo.

Kocha wa Tanzania afunguka

Kocha wa Tanzania, Majuto Majaliwa alisema msimu huu maandalizi ya muda mrefu ndiyo yamewapa matokeo chanya.

“Kuna wakati tulikuwa tunaonekana kama wasindikizaji, lakini sasa hamasa imeonekana, vipaji vipo ni jukumu la kuviendeleza na kuhakikisha hapa tulipofika haturudi chini.

“Tusipoteze tena muda kwenye mashindano kama haya, tuwape vijana nafasi,” aliongeza.

Shelisheli waongoza unadhifu

Shelisheli licha ya kutofanya vizuri ni timu pekee ambayo ilikuwa nadhifu muda wote wa mashindano hayo yaliyoshirikisha timu nane wakifuatiwa na Rwanda.

“Ni kawaida yetu kuwa kwenye uniform (sare) ya rangi ya bendera ya nchi yetu kila tunapokuwa kwenye mashindano ya kimataifa,” alisema Michael Gomme.