Cheki hili chama la PSG litakavyokuwa Neymar akiondoka

Friday August 16 2019

 

PARIS, UFARANSA. PARIS Saint-Germain wanakaribia kumsuma nje ya kikosi chao supastaa, Neymar lakini kama lisemwalo ni kweli, basi jambo hilo litawafanya kutengeneza kikosi matata kabisa kitakachosumbua Ufaransa na Ulaya kwa ujumla.

Real Madrid na Barcelona ndizo zinazotajwa kuhitaji huduma ya Neymar na kwenda hilo, mpango uliopo ni kwamba kila timu ipo tayari kutoa mastaa wake watatu ili kunasa huduma ya Mbrazili huyo. Barcelona imedaiwa kuwa tayari kumtoa Ousmane Dembele, Ivan Rakitic na Philippe Coutinho kwenye dili hilo, wakati wenzao Real Madrid wameripotiwa kuwa tayari kumtoa Isco, Raphael Varane na Marcelo.

Na hilo ni kweli, basi vyovyote itakavyokuwa, PSG watakuwa wametengeneza kikosi kimoja matata kabisa kitakachokuwa tishio na pengine kuliko Barcelona au Real Madrid moja wapo itakayofanikiwa kunasa huduma ya Neymar.

Neymar amekuwa kwenye kikosi cha PSG miaka miwili tu tangu aliponaswa kwa ada ya Pauni 198 milioni mwaka 2017 na hivyo kuweka rekodi ya kuwa mwanasoka ghali kabisa duniani. Kwenye kikosi hicho cha PSG, alitengeneza kombinesheni matata kwenye safu ya kushambulia sambamba na Kylian Mbappe na Edinson Cavani.

Lakini, kama ataondoka kwenye Barcelona na wao wakafanikiwa kuwanasa Coutinho, Rakitic na Dembele basi watakuwa wamepiga bao la maana, wakati kama akienda Madrid,  kwa kubadiliana na Isco, Varane na Marcelo, basi watakuwa ametengeneza kikosi kitakachowafanya kuwa na nguvu zaidi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Advertisement