Cheki Wakali wa pasi za mabao England

Muktasari:

  • Hawa hapa ndio mafundi wa kupiga mabao wanaongoza kwa asisti kwenye Ligi Kuu England kwa kuanzia mwanzoni mwa msimu uliopita hadi sasa msimu ukiwa umefika katikati. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Transfermarkt.

LONDON, ENGLAND.LIGI Kuu England kwa msimu huu imeshaingia kwenye duru la pili na kila kitu kimeonekana wazi kwenye mbio za kila kitu kwa timu na mchezaji mmojammoja.

Mabao yamekuwa yakitiririka, mastraika wapo bize kuweka mipira nyavuni, lakini kuna wanaume matata kabisa ambao wao kazi yao ni kupika hayo mabao wanayofunga kina Harry Kane na Sergio Aguero.

Hawa hapa ndio mafundi wa kupiga mabao wanaongoza kwa asisti kwenye Ligi Kuu England kwa kuanzia mwanzoni mwa msimu uliopita hadi sasa msimu ukiwa umefika katikati. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Transfermarkt.

5.Paul Pogba - 17

Baada ya kuwa kwenye kipindi kigumu sana cha uchezaji wake chini ya kocha Jose Mourinho, hatimaye staa wa Manchester United, Paul Pogba, ameonekana kurudi kwenye ubora wake na kucheza soka analotaka akiwa chini ya kocha wa muda, Ole Gunnar Solskjaer. Kiungo huyo Mfaransa kwa sasa amepiga jumla ya asisti saba kwenye Ligi Kuu England kwa mechi 19 alizocheza hadi sasa, huku asisti nne akizipiga kwenye mechi tano za karibuni. Pogba kwa sasa anacheza soka ambalo mwenyewe anaweza analifurahia kwa sababu linampa uhuru wa kuitumikia klabu hiyo ya mapenzi yake huko Old Trafford.

Asisti msimu uliopita: 10

Jumla ya mechi: 46

4.Christian Eriksen - 18

Ukitaja kikosi cha Tottenham Hotspur, basi moja kwa moja akili yako itakupeleka kwa mshambuliaji Harry Kane kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao.

Lakini, hapo utakuwa umesahau ufundi wa mpishi mmoja matata kabisa wa mabao hayo, Christian Eriksen, ambaye ndiye hasa anayefanya mambo makubwa katika kumfanyia wepesi Kane kufunga mabao.

Kutokana na hilo ndio maana hakionekani ni kitu cha ajabu kusikia Eriksen yupo kwenye orodha ya wachezaji wanaosakwa na Real Madrid kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kiungo huyo wa kimataifa wa Denmark yupo kwenye kiwango bora kabisa msimu huu akifunga mabao manne na kuasisti mara saba katika mechi 19 alizocheza.

Asisti msimu uliopita: 11

Jumla ya mechi: 56

3.Mohamed Salah - 19

Mohamed Salah aliweka rekodi nyingi sana kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita kupitia ule mguu wake matata kabisa kabisa wa kushoto.

Kiwango chake bora ndani ya uwanja kiliifanya Liverpool kufanya vizuri na msimu huu anaendelea kucheza soka la juu kabisa kuwafanya wababe hao wa Anfield kushuka usukani kwenye ligi. Msimu huu, Mo Salah amefunga mabao 14 na kuasisti mengi manane katika mechi 22 alizocheza kwenye Ligi na hivyo kuwa mmoja wa wachezaji waliohusika kwenye mabao mengi tangu mwanzoni mwa msimu uliopita.

Asisti msimu uliopita: 11

Jumla ya mechi: 58

2.Raheem Sterling - 22

Baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018, Raheem Sterling ameonyesha ubora wake mkubwa sana kwenye Ligi Kuu England.

Manchester City wanakimbizana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England wakikimbizana na Liverpool msimu huu. Moja ya wachezaji wanaofanya kikosi cha Man City kuwa na ubora mkubwa ndani ya uwanja ni Sterling. Mwingereza huyo alifunga mabao tisa na kupiga asisti saba katika mechi 19 alizocheza kwenye ligi hiyo msimu huu.

Asisti msimu uliopita: 15

Jumla ya mechi: 52

1.Leroy Sane - 24

Licha ya kuanza vibaya mwanzoni mwa msimu huu, Leroy Sane ameanza kurudi kwenye makali yake kama yale aliyokuwa nayo msimu uliopita. Wakati Kevin De Bruyne akikosekana kwenye kikosi cha Manchester City, kina huyo wa Kijerumani ameonyesha uwezo mkubwa katika kufunga na kupika mabao mengine. Msimu huu amepiga asisti nane na kufunga mara saba katika mechi 20 alicheza kwenye Ligi Kuu England.

Asisti msimu uliopita: 15

Jumla ya mechi: 52