Cheki Big Six zinavyopiga pesa kupitia wachezaji wa akademia

Muktasari:

  • Akademia imekuwa ni chanzo kikubwa cha mapato kwa klabu duniani kutokana na kuuza wachezaji pamoja na kuwatumia

LONDON, ENGLAND. LIGI Kuu England inarudi wikiendi hii baada ya kupisha mechi za kimataifa kwa kipindi cha wiki mbili. Mashabiki wa soka walipata uhondo wa michuano ya UEFA Nations League na ile ya kufuzu kwa Afcon 2019 kwa kipindi hicho cha wiki mbili, kabla ya utamu wao wa Ligi Kuu England kurudi upya wikiendi hii. Kwenye Ligi Kuu England kuna klabu zinazofahamika kama Big Six kwa maana ya Manchester City, Manchester United, Arsenal, Chelsea, Tottenham Hotspur na Liverpool.
Timu hizo zimekuwa na ushindani wa aina tofauti kuanzia kwenye matokeo ya uwanjani hadi kwenye mambo mengine ya nje ya uwanja. Kwenye makala haya, yanahusu ni klabu gani hapo iliyopiga pesa nyingi  kutokana na mauzo ya kuwauza wachezaji waliohitimu kutoka kwenye akademia zao.

6.Liverpool- Pauni 3.3 milioni
Liverpool inahitaji kuifanyia mabadiliko makubwa akademia yao kwa sababu haizalishi wachezaji wengi wenye uwezo wa kuchaguliwa na kuja kufanya kweli kwenye kikosi chao cha kwanza. Trent Alexander-Arnold ameibukia kutokea kwenye akademia hiyo ya Melwood, lakini amekuwa mchezaji mmoja tu baada ya miaka mingi kupita. Kutokana na hilo ndio maana haionekani kuwa ni ajabu kwa Liverpool kuwa timu ya mwisho kwenye ile Big Six kupata faida kiduchu kutokana na mauzo ya makinda wao waliohitimu kutoka kwenye akademia yao. Liverpool imeingiza Pauni 3.3 milioni tu kwenye mauzo hayo na wachezaji wao walitokea kwenye akademia yao.

5.Chelsea- Pauni 6.5 milioni
Chelsea imekuwa timu maarufu kwa kutoa wachezaji wengi kwa mkopo kwenye Ligi Kuu England. Hata hivyo, wakali hao wa Stamford Bridge wameingiza Pauni 6.5 milioni kutokana na mauzo ya wachezaji wake waliohitimu kutoka kwenye akademia yao. Kumekuwa na ripoti kwamba Uefa na Fifa imepanga kuweka msimamo wa idadi ya wachezaji wanaotolewa kwa mkopo. Kutokana na hilo, Chelsea watakuwa kwenye wakati mgumu wa kuwatema makinda wao waliowasambaza kwenye klabu nyingi tofauti huko Ulaya.

4.Man United- Pauni 9.7 milioni
Manchester United ilipata mafanikio makubwa sana kwenye Ligi Kuu England wakati ilipokuwa chini ya Sir, Alex Ferguson, ambapo kikosi hicho kilikuwa kikipandisha wachezaji viwango kutoka kwenye akademia yao. Mwaka 1992, klabu hiyo iliwapandisha wachezaji kama Ryan Giggs, Paul Scholes, Gary Neville, Phil Neville, Nicky Butt, David Beckham na wengineo kutoka kwenye akademia yao. Lakini, kwa sasa klabu hiyo inaburuzwa na mahasimu wao, Manchester City katika upande huo wa kufua wachezaji kutoka kwenye akademia yao. Kipindi ambacho Man United inazalisha wachezaji wengi walikuwa wakipandishwa na kucheza kikosi cha kwanza. Kuna wale wengine waliouzwa baada ya kuhitimu tu kutoka kwenye akademia hiyo na kuwafanya Man United kuvuna Pauni 9.7 milioni kwenye mauzo yao. Baadhi ya wachezaji walioibua kwenye akademia na kuechezea timu hiyo kwa sasa ni pamoja na Paul Pogba, Scott McTominay, Marcus Rashford na Jesse Lingard.

3.Arsenal- Pauni 11.6 milioni
Falsafa za Arsene Wenger kwa miaka yake 22 aliyodumu kwenye soka imekuwa yakizalisha makinda matata kabisa kutoka kwenye akademia ya timu hiyo na kisha kuwapandisha kwenye kikosi cha kwanza. Kuna wachezaji wengi walitokea kwenye akademia kabla ya kupandishwa na kuwa wachezaji muhimu kwenye klabu hiyo na miongoni mwao ni Aaron Ramsey, Holding na Alex Iwobi kwa kuwataja kwa uchache. Licha ya kupandisha wachezaji kwenye kikosi chao cha kwanza, Arsenal imeuza wakali wake wengine waliotokea kwenye akademia na kuingiza kiasi cha Pauni 11.6 milioni klabuni na kuwafanya kuwa klabu namba tatu kwenye Ligi Kuu England iliyopata pesa nyingi kwa kuwauza wachezaji wake waliohitimu kutoka kwenye akademia yao.

2.Tottenham- Pauni 11.7 milioni
Tottenham Hotspur imekuwa na akademia bora kabisa kwenye Ligi Kuu England kwa sasa. Kupitia akademia hiyo, Spurs imepandisha wachezaji wengi kwenye kikosi chao cha kwanza kwa miaka ya karibuni. Baadhi ya wachezaji waliotokea kwenye akademia yao na kufanya vizuri kwenye kikosi cha kwanza ni pamoja na Harry Kane, Kieran Trippier, Danny Rose, Harry Winks na Walker-Peters. Klabu hiyo pia imevuna Pauni 11.7 milioni kutokana na kuwauza mastaa wake waliotokea kwenye akademia zao. Mashabiki wa Arsenal hawataamini hili kwamba wapinzani wao wa London wamekuwa wakizalisha wachezaji mahiri zaidi kutoka kwenye akademia yao na kuwapatia pesa za kutosha kuliko wao.

1.Man City- Pauni 70.6 milioni
Mmiliki wa Manchester City, bilionea, Sheikh Monsour si kwamba amewekeza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo baada ya kuichukua 2008 bali amewekeza kwenye akademia ya timu hiyo kwa kufunga vifaa vya kisasa kabisa vya mazoezi na kuweka mazingira bora. Klabu hiyo imekwenda kuchukua makinda bora kutoka katika klabu nyingine na kuwaweka kwenye akademia yao na hakika mavuno yake ni makubwa. Kutokana na hilo, Man City imeweza kutengeneza makinda bora na kuingiza kiasi cha Pauni 70.6 milioni katika mauzo hayo ya makinda wake kutoka kwenye akademia. Mmoja wa makinda hao ni Jadon Sancho, aliyeuzwa kwenda Borussia Dortmund kwa Pauni 8 milioni. Makinda wengine ni kipa Angus Gunn, aliyeuzwa Southampton kwa Pauni 13.5 milioni, Jason Denayer kwenda Lyon kwa Pauni 11.8 milioni, Rony Lopes amekwenda Monaco kwa Pauni 9 milioni na Pablo Maffeo amesajiliwa na Stuttgart kwa Pauni 8.1 milioni. Hivyo ndivyo akademia ya Man City ilivyoingiza pesa.