Cheka arudi, kuzichapa Desemba

Dar es Salaam. Bondia bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka amerejea na kuanza maandalizi ya ulingoni.

Cheka, ambaye alihamishia makazi nchini Msumbiji tangu Desemba 2018, amerejea na kuweka kambi Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Cheka alisema: “Nimerudi kuishi Tanzania, ingawa sasa maisha yangu yatakuwa ni Dar.

“Nimeanza mazoezi, najifua kwenye kambi ya ngumi Chamazi, najiandaa kucheza pambano Desemba, hapa hapa Dar,” alisema bondia huyo.

Alisema atazichapa na bondia kutoka nje ya nchini, ambaye bado wako kwenye mazungumzo na menejimenti ya Cheka Promotions na yatakapokamilika atamuweka wazi.

“Desemba narudi ulingoni, mashabiki wangu wamekuwa wakiniuliza mara kwa mara kama nimeacha ngumi au la!, niliamua kupumzika, ngumi hazina kustaafu, ndiyo sababu leo hii tunamsikia Mike Tyson anataka kurudi ulingoni.

Bondia huyo mwenye miaka 36 anasema bado ana muda zaidi wa kuonekana ulingoni na kutoa burudani kwa mashabiki wake, ambao waliikosa tangu Desemba 26, 2018 alipochapwa kwa Knock Out (KO) na Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’.

Bondia huyo ambaye alihamishia makazi yake nchini Msumbiji alikozaliwa mama yake mzazi, alisema ameamua kurudi nyumbani Tanzania alikozaliwa yeye.