Chanzo tenisi kukosa timu ya taifa chaanikwa

Thursday May 21 2020

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Sababu inayopelekea timu ya taifa ya mchezo wa Tenisi nchini kukosekana hadi kupelekea kupotea kwa kundi kubwa la vijana wenye vipaji vya mchezo huo, imeanikwa.

Kundi kubwa la wachezaji bora vijana wa mchezo huo limekuwa likikimbilia katika ukocha au kujihusisha na shughuli nyingine kutokana na kutokuwepo kwa timu ya Taifa.

 Tanzania ni moja ya nchi za Afrika Mashariki zenye timu bora ya vijana ambayo mwaka jana ilitwaa nafasi ya pili kwenye mashindano ya Afrika Mashariki na Kati yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

 "Tuna changamoto ya kutokuwa na timu ya taifa ya wakubwa ambayo imedumu kwa muda mrefu," anasema Mwenyekiti wa Chama cha Tenisi Tanzania (TTA), Denis Makoi.

Anasema changamoto hiyo imetokana na kutoshiriki mashindano ya Davis Cup ambayo yanatambuliwa na Shirikisho la Tenisi la Kimataifa (ITF).

"Tulijaribu kuomba, ingawa hadi kuruhusiwa kuingia huko na timu yetu ya Taifa itambulike ni mlolongo mrefu, mwaka huu ITF ilisema tutapigiwa kura, na kura zikitosha basi mwaka 2021 tutaruhusiwa kwa mara ya kwanza tutatambulika kuwa na timu ya Taifa ya wakubwa," amesema.

Advertisement

Amesema kama wataruhusiwa, TTA itapaswa kulipa dola 5600 kama ada na Tanzania itapangiwa nchi ambazo zitacheza nazo ili timu hiyo kuingia kwenye viwango vya ubora.

Kocha wa timu ya Taifa ya Tenisi ya vijana, Salum Mvita amesema changamoto kubwa iko kwenye ada.

"Kule kwenye timu ya vijana uwa wanalipia dola 600, kila mwaka tunalipa, lakini huku kwa wakubwa kidogo ada ni changamoto," anasema.

Anasema wakati wa uongozi wa Inger Njau alijaribu kupambana ili timu ya wakubwa ya Taifa irambulike kimataifa, lakini hakukamilisha hilo akaondolewa madarakani.

"Uongozi uliokuja haukuangaika nalo, japo tuliwapigia kelele lakini hawakufanya. Uongozi wa sasa umeanza kulifuatilia, lakini tuna changamoto kubwa, vijana tunaowafundisha sasa wakifikisha miaka 17 wanakuwa hawana pa kwenda, hivyo wanalazimika kucheza mashindano ya humu humu nchini au kuwa makocha,".

Katika historia ya tenisi nchini, Tanzania imetajwa kutokuwa na timu ya taifa ya wakubwa zaidi ya ile ya vijana ambayo licha ya kufanya vizuri, maisha yao ya tenisi huwa mafupi kwani wanapofikisha miaka 18 safari yao inakuwa imeishia hapo katika mchezo huo.

Advertisement