Chanzo cha Morrison kudakwa na polis Dar hiki hapa

Muktasari:

MATUKIO ya utata yanazidi kumuandama winga wa Yanga, Bernard Morrison baada ya jana kukamatwa na polisi kisha kuachiwa baadaye.

MATUKIO ya utata yanazidi kumuandama winga wa Yanga, Bernard Morrison baada ya jana kukamatwa na polisi kisha kuachiwa baadaye.

Tukio hilo lilitokea mchana wa jana na kuthibitishwa na jeshi hilo la Polisi, ilielezwa Morrison alikutwa na mkasa huo baada ya askari wa doria kulitia shaka gari lake, lililokuwa limeegeshwa maeneo yasiyoruhusiwa.

Chanzo kimoja kilidai, askari hao walisimama na kutaka waliopo garini wafungue na ndipo Morrison akakutwa na rafiki zake na baada ya mahojiano polisi hawakuridhika na maelezo ya winga huyo Mghana na kutaka kulipekua gari naye kuzua utata kwa kuwagomea.

“Askari walihisi harufu ya kitu kutoka ndani ya hiyo gari sasa walipotaka kumfanyia upekuzi akagomea upekuzi huku akileta utata akitaka kuwarekodi polisi, kilisimulia chanzo hicho. Hata hivyo, askari walimng’ang’ani na kuondoka nao kwenda kutoa maelezo yake kituo cha Polisi Oysterbay.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Edward Bukombe alithibitisha kushikiliwa kwa muda kwa winga huyo.

“Ni kweli hilo tukio lipo, tulikuwa naye Morrison hapa kituoni alikamatwa na vijana wetu waliokuwa doria huko barabarani na wakamfikisha hapa. Walitofautiana huko wakaamua kumleta hapa kwa kumchukua maelezo lakini akatoa maelezo na kuachiwa,” alithibitisha Kamanda Bukombe.

Morrison amekuwa nje ya kikosi cha Yanga kwa muda mrefu tangu baada ya kufanyiwa ‘sub’ katika mchezo dhidi ya Simba na kuondoka moja kwa moja uwanjani, amekuwa na matukio mbalimbali ambayo yamekuwa yakileta utata.