Chanongo aipasha Mtibwa yaifuata KCCA

Muktasari:

Mtibwa Sugar imefuzu kucheza na KCCA baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 5-1 dhidi ya Northern Dynamo

Shelisheli. Bao pekee la Haruna Chanongo limetosha kuipa Mtibwa Sugar ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Northern Dynamo na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1.

Mtibwa Sugar inayoshiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 10 imefanikiwa kusonga mbele na sasa itacheza na KCCA ya Uganda katika hatua inayofuata.

Katika mchezo huo wa ugenini Mtibwa Sugar ilisubiri hadi dakika 58, kupata bao pekee lililofungwa na Chanongo na lilitosha kuwapeleka katika raundi ya pili.

Baada ya mchezo huo Mtibwa Sugar imepanga kurudi jijini Dar es Salaam kesho Jumatano tayari kwa maandalizi ya mchezo huo na KCCA.

Mtibwa Sugar sasa watakuwa na kibarua kizito dhidi ya KCCA katika mechi itakayochezwa ugenini kati Desemba 14 na mchezo wa marudiano utacheza Dar es Salaam Desemba 21.