Chanongo: Sarpong hatari

WINGA wa Mtibwa Sugar, Haruna Chanongo amesema kiwango alichokionyesha straika wa Yanga, Michael Sarpong katika mechi yao, waliopigwa bao 1-0 ni tishio.

Chanongo alisema licha ya Sarpong kutokufunga bao katika mchezo huo, ndiye alikuwa mwiba kwa mabeki wao kutumia muda mwingi kumzibia mianya ya kuwadhuru, ndipo Lamine Moro alipata upenyo wa kuwaumiza.

“Ni mchezaji hatari, jamaa ni mpambanaji na analazimisha mashambulizi, akiendelea hivyo ataisaidia timu yake kufunga mabao mengi na atakuwa chachu kwa wazawa kwani lazima mchezaji wa kigeni awe na kitu cha tofauti na wenyeji wake,” alisema Chanongo na kuongeza.

“Ni kweli hakufunga lakini niliona namna ambavyo alikuwa anafanya mabeki wetu muda mwingi wawe wanamkaba ndio maana Moro alijiongeza na kufunga, ingawa ulikuwa mchezo mgumu na tulicheza kwa nidhamu ya hali ya juu,” alisema.

Alisema ligi ikiwa na ushindani anaamini inakuwa nzuri, kwani kila mchezaji anakuwa anapambana kwa ajili ya kuisaidia timu yake na kuona kila mechi inakuwa kama fainali.

“Ujue hizo Simba na Yanga zikikutana na ushindani mkali basi zitakuwa zinaheshimu kila mechi, ndio maana nimetolea mfano wa Sarpong namna ambavyo alikuwa anapambana bila kukata tamaa ya kuona anakabwa kwa umakini,” alisema.

Mbali na kumzungumzia Sarpong alisema kwa wachezaji wengine wa kigeni ambao anaona watakuwa na amsha amsha kwenye ligi ni Clatous Chama kiungo wa Simba ambaye alisema anajua anachokifanya uwanjani.