Chambua awapa neno Serengeti Boys

Friday March 15 2019

 

By CHARITY JAMES

MCHEZAJI wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa Taifa Stars, Sekilojo Chambua amesema licha ya timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 'Serengeti Boys' kutolewa mapema kwenye mashindano ya UEFA Assist yaliyofanyika Uturuki, bado ina nafasi ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Afcon itakayoanza kutimua vumbi mwezi ujao.
Ikiwa nchini Uturuki, Serengeti Boys ilicheza mechi tatu na kushinda mmoja huku ikipoteza miwili mbele ya Guinea kwa kuchapwa bao 1-0, kisha wakaichapa Australia mabao 3-2 na baadaye kumaliza na Uturuki, ambao walishusha mvua ya bao 5-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chambua alisema maandalizi ya Serengeti Boys Uturuki ni kipimo kizuri na wanaweza kuyatumia kama changamoto kwa kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kabla ya mashindano hayo.
"Uturuki wamekutana na timu ambazo zina maandalizi mazuri na makubwa zaidi yao, wamepewa changamoto kwa kufungwa na kutolewa mapema, hivyo ni muda wa mwalimu kutumia makosa aliyoyaona kwa kuhakikisha anayasawazisha kabla hawajaanza mashindano ya Afcon na wao wakiwa kama wenyeji.
"Tuna timu nzuri inapambana na inafundishika, naamini bado tuna nafasi nzuri ya kutumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani kwa kutwaa taji la mashindano hayo, Watanzania tunatakiwa kuungana pamoja kuwapa ushirikiano wachezaji wetu ili waweze kufanikisha hili," alisema.
"TFF na benchi la ufundi wanatakiwa kuwaanda kisaiokolojia hawa vijana na kuwaanimisha, kutolewa kwao mapema sio hatua mbaya wala njia ya kufanya vibaya kwani, wao bado ni bora uwanjani," alisema.
Tanzania itakuwa mwenyeji katika mashindano ya Afcon yanayoanza Aprili, mwaka huu na Serengeti Boys iko kundi A ikiwa na timu za Nigeria, Angola na Uganda.

Advertisement