Chambua amchambua Molinga

Muktasari:

Molinga ameendelea kufanya maajabu kwenye mechi za kirafiki, baada ya kutupia juzi dhidi ya Pamba, amefunga mengine mawili katika mechi inayoendelea kati ya Yanga na Toto Afrika, Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Dar es Salaam. Mchezaji wa zamani wa Yanga,  Sekilojo Chambua amesema kitendo cha David Molinga kufunga kwenye mechi za kirafiki kinaijenga akili yake kujiamini kuelekea mechi na Zesco ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Inamuongezea kujiamini kwa sababu mshambuliaji ni lazima alione gori, hiki ni kitu kizuri kwake na kitamsaidia kufanya vyema ligi ya Mabingwa na ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara"amesema.
Pia amezungumzia mechi ambazo Yanga inacheza kujiandaa na Zesco kwamba haoni picha kamili ya uhalisia wa mechi yao ya kimataifa.
"Japokuwa ni mipango ya klabu lakini nikitazama kiundana naona kama haileti picha halisi ya kile ambacho wanakwenda kukifanya siku ya Jumamosi"
"Jambo ninaloweza kushauri kocha Mwinyi Zahera aendelee kuwaaminisha wachezaji kwamba wanaweza na naamini ni mtaalamu kwa hilo, kila kitu kinawezekana kwa kujituma,"amesema.
Molinga raia wa DR Congo,ameanza kuonyesha makali yake, alianza kufunga dhidi ya Pamba timu yake ikitoka sare ya bao 1-1, na ameishatupia mabao 2-0 dhidi ya Toto Africa, mchezo unaoendelea Nyamagana, Mwanza.
Yanga ipo mbele ya mabao 2-0 dhidi ya Toto dakika 45 za kipindi cha kwanza, Molinga akiwa ndiye aliyewanyenyua mashabiki kwa mabao yote mawili.
Molinga hakuwa na mwanzo mzuri alipojiunga na Yanga,akageuka kituko mtandao na sasa ameanza kuzima kejeli za mashabiki taratibu.