Chama bora la msimu hadi sasa

Muktasari:

Hawa ndio wachezaji 11 wanaounda kikosi cha kwanza ambao wamefanya vyema kwenye Ligi Kuu tano Bora huko Ulaya hadi kufikia sana msimu huu

HUKO kwenye Ligi Kuu tano bora za Ulaya, Ufaransa ndiyo iliyoshuhudia mechi nyingi hadi sasa, mechi tisa. Kwa kifupi tu hakuna ligi iliyofikisha mechi 10 kati ya hizo tano bora, ambazo ni Ligi Kuu England, La Liga, Ligue 1, Bundesliga na Serie A.
Lakini, kwa mechi hizo tu chache zilizochezwa, kuna wachezaji wameonyesha kiwango kikubwa sana ndani ya uwanja na kama utapewa kazi ya kuchagua Kikosi cha Kwanza cha msimu huu kwa mechi ambazo zimeshachezwa kwenye ligi hadi sasa, hivi ndivyo litakavyokuwa chama hilo.

1.Tomas Vaclik
KIPA
(Sevilla)
Kipa Tomas Vaclik alijiunga Sevilla akitokea FC Basel kwa ada ya Euro 6.3 milioni katika dirisha lililopita na huduma yake hakika imeonekana pesa iliyotumika kupata saini yake kama imekuwa bure. Kipa huyo wa kimataifa wa Jamhuri ya Czech amefanya sevu 57 na amecheza mechi zaidi ya sabab bila ya kuruhusu mpira kutinga kwenye nyavu zake na kuwa kipa mahiri zaidi kwenye ligi tano bora za Ulaya. Anakipiga huko kwenye La Liga.

2.Joao Cancelo
BEKI WA KULIA
(Juventus)
Inter Milan wamepoteza, Juventus wameingiza. Beki wa kulia wa zamani wa Valencia, Joao Cancelo amekuwa mtu muhimu huyo Turin msimu huu baada ya msimu uliopita kucheza kwa mkopo San Siro. Mreno huyo amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Juventus, ambapo alikuwamo kwenye kikosi katika mechi zote ilizocheza timu hiyo bila ya kuruhusu bao  kwenye wavu wao. Cancelo pia ni fundi wa kukokota mpira na kocha Max Allegri kwake ni raha tu.

3.Jordi Alba
BEKI WA KUSHOTO
(Barcelona)
Pengine Luis Enrique anamwona hana nafasi kwenye kikosi chake cha Hispania, lakini Jordi Alba bado ni mmoja wa mabeki wa kushoto bora kabisa duniani kutokana na kile anachokifanya msimu huu. Beki huyo amehusika kwenye asisti nyingi sana msimu huu, akiwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha Barcelona kutokana na kupiga asisti nne. Ukitakiwa kuchagua kikosi cha msimu kwa mechi zilizocheza hadi sasa, Alba hawezi kukosa.

4.Virgil van Dijk
BEKI WA KATI
(Liverpool)
Virgil van Dijk ni mmoja wa mabeki mahiri kabisa huko Ulaya kwa sasa. Huduma yake kwenye kikosi cha Liverpool imekuwa kitu muhimu na kuituliza timu hiyo kuwa kwenye wakati mzuri wa kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri ndani ya timu hiyo. Kiwango chake huko Anfield kimekuwa majibu tosha kwanini kocha Jurgen Klopp alilipa Pauni 75 milioni kupata saini yake. Van Dijk ni bonge la beki.

5.Kalidou Koulibaly
BEKI WA KATI
(Napoli)
Napoli hawakufanya usajili mkubwa kwenye dirisha lililopita, lakini jambo la maana walilolifanya ni kumbakiza beki wao wa kati Kalidou Koulibaly, ambaye alikuwa akisakwa kwa nguvu zote na vigogo wa Ulaya. Shughuli ya beki huyo si ya kitoto na ndiyo maana haishangazi bado anawindwa na timu kubwa zaidi za Ulaya ikiwamo Barcelona. Kwa msimu huu ameisaidia Napoli kucheza mechi kibao bila ya kuruhusu mpira kutinga kwenye nyavu zao.

6.Allan
KIUNGO WA KATI
(Napoli)
Kumpoteza Jorginho kwenye dirisha la majira ya kiangazi kulikuwa pigo kubwa kwenye kikosi cha Napoli, lakini kiwango cha kiungo Allan kumeondoa majungu makubwa kwenye kikosi hicho. Kiungo, Allan alikuwa moto kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool na kocha Carlo Ancelotti anaonekana kumwaamini zaidi na kumpa nafasi. Ni Mbrazili, lakini kocha wa Italia, Roberto Mancini anataka kumpa nafasi katika kikosi cha Azzurri.  

7.Kylian Mbappe
KIUNGO WA KULIA
(PSG)
Ni kinda matata zaidi kwenye soka la Ulaya kwa sasa. Kylian Mbappe akiwa na umri wa miaka 19 tu tayari ameishikilia dunia kutokana na kiwango chake cha soka anachokionyesha huko kwenye Ligi Kuu Ufaransa na timu ya taifa ya nchi hiyo, Les Bleus. Mbappe amefunga mabao 10 katika mechi saba tu alizoichezea Paris Saint-Germain msimu huu, ikiwamo mabao yake manne aliyofunga ndani ya dakika 13 dhidi ya Lyon.

8.Jorginho
KIUNGO WA KATI
(Chelsea)
Uamuzi wa Jorginho kufuatana na Maurizio Sarri huko Chelsea wakati walipoondoka Napoli badala ya kumfuata Pep Guardiola huko Manchester City umekuwa mzuri kutokana na kiwango bora anachokionyesha kwenye kikosi hicho cha Stamford Bridge kwa msimu huu. Jorginho amekuwa moto wa kiungo ya Chelsea kwa sasa akiongoza kwa kupiga pasi huku timu yake ikiwa haijapoteza mechi yoyote kwenye Ligi Kuu England hadi sasa.

9.Krzysztof Piatek
MSHAMBULIAJI
(Genoa)
Hakika Krzysztof Piatek yupo kwenye ubora wake kutokana na kuikamatia Serie A patamu. Piatek amekuwa moto tangu alipojiunga na Genoa akitokea Cracovia kwa ada ya Euro 4.5 milioni tu kwenye dirisha lililopita la usajili. Ni staa wa kimataifa wa Poland na amekuwa akifunga hata kwenye timu yake ya taifa. Kwenye Serie A amefunga mabao tisa na saini yake inasakwa na Barcelona.

10.Lionel Messi
KIUNGO MSHAMBULIAJI
(Barcelona)
Umri wake ni miaka 31, lakini huduma yake ndani ya uwanja haijawahi kushuka. Lionel Messi ni mchezaji asiyefilisika mawazo ya kiuchezaji na mbinu za ndani ya uwanja ambapo huduma yake matata imekuwa kitu cha msingi katika kikosi cha Barcelona hasa kwa msimu huu. Staa huyo amefunga mabao 11 katika mechi 11 za michuano yote aliyocheza msimu huu huku akiwa na asisti tano pia.

11.Eden Hazard
KIUNGO WA KUSHOTO
(Chelsea)
Kwenye Ligi Kuu England, Eden Hazard amekuwa hatari kweli kweli. Chini ya Maurizio Sarri amepewa kazi moja tu ya kuchambulia, kukaba watafanya wengine na ndio maana amefunga mabao saba hasi sasa kwenye ligi hiyo. Kama utatakiwa kuchagua kikosi cha msimu kwa mechi zilizochezwa hadi sasa, Hazard hawezi kukosa nafasi kwenye timu hiyo. Kiwango chake hadi Real Madrid wamepagawa kutaka saini yake.


KOCHA
Max Allegri
JUVENTUS


SUMMARY
Hawa ndio wachezaji 11 wanaounda kikosi cha kwanza ambao wamefanya vyema kwenye Ligi Kuu tano Bora huko Ulaya hadi kufikia sana msimu huu
...