Chama awaponza maafande wa Zenji

Tuesday January 8 2019

 

KOCHA Mkuu wa KMKM, Ame Msimu amekiri wazi kwamba aliandaa jeshi maalum la kuidhibiti Simba na hasa Clatous Chama, lakini bahati mbaya walipoteza kutokana na udambwidambwi wa kiungo huo fundi.

KMKM walikubali bao la jioni kwenye mchezo huo na kulala 1-0, licha ya kuonyesha soka la ushindani na kuwabana kwa muda mrefu nyota wa Msimbazi, japo Chama kama kawaida yake aliendelea kuthibitisha kuwa hajakuja nchini kuuza sura.

Kocha Msimu alisema wanakubali Simba ni timu kubwa na ina wachezaji bora hivyo kwa timu pinzani ni lazima ijipanga na iwe na kikosi kizuri kupambana na muziki wa Wekundu hao.

Alisema nyota aliokuwa anawahofia kuwaumiza Chama na kwamba aliwaelekeza wachezaji wake jinsi ya kucheza naye kwa tahadhali kubwa ili asifike langoni kwao.

“Chama tulimfuatilia na tuliona uwezo wake, ni mchezaji mzuri na usipokuwa makini anakuliza muda wowote, mbali na Chama kikosi kizima cha Simba kina wachezaji wazuri ambao muda wowote wanakudhuru, anajuwa anachokifanya tena muda wowote mtu usioutegemea huyo anastahilii kuitwa ‘proo’.

“Kikosi kilichocheza na Simba kwa asilimia kubwa kilikuwa na wachezaji ambao sikuwatumia mechi yetu na Mlandege, kwenye kikosi cha awali nilichukuwa wachezaji wanne tu ndiyo niliwaongeza kucheza na Simba ingawa mipango yetu ilifeli,” alisema. Alisema wanapambana kuona mechi yao ya leo dhidi ya Chipukizi wanapata alama tatu. Simba inaongoza Kundi A ikiwa na alama sita, ikifuatiwa na Mlandege yenye alama nne kisha KMKM yenye pointi moja na Chipukizi ikiwa imeshaaga mashindano.

Advertisement