Chama awapa mzuka mashabiki Simba

Muktasari:

Katika mchezo wa jana JS Saoura waliongoza kwa bao moja muda mwingi wa mchezo kabla ya Al Ahly kusawazisha dakika ya 89.

Kiungo fundi wa Simba,Clatous Chama ni kama amewapa mzuka wachezaji wenzake na mashabiki wa klabu hiyo wanaoisubiri kwa hamu mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu hiyo na AS Vita  ya Congo.
Mechi hiyo itakayoanza majira ya saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania ni muhimu kwa Simba kushinda ili  kuongoza kundi D kwani  kama itashinda itakuwa imejikusanyia pointi sita.
Chama ametamka kuwa  iwe kwa ndoano au kiboko lazima As Vita wapasuke leo na kuzidi kujiwekea mazingira mazuri na kutimiza malengo yao ya kucheza nusu fainali na fainali msimu huu.
Kiungo huyo raia wa Zambia amejizolea umaarufu mkubwa kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo na hata wa timu nyingine hapa nchini kutokana na kiwango bora anachokionyesha uwanjani katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu Bara na Mashindano ya Kimataifa.
Al Ahly ya Misri ndio inaongoza kundi D ikiwa na pointi nne baada ya sare ya jana Ijumaa kutoka sare ya bao 1-1 na JS Saoura ya Algeria, Simba inafuatia ikiwa na pointi 3 wakati  JS Saoura ya tatu ikiwa na pointi moja na As Vita inashika mkia ikiwa haina pointi  kabla ya mecho wa leo jioni.
Katika mchezo wa jana JS Saoura waliongoza kwa bao moja muda mwingi wa mchezo kabla ya Al Ahly kusawazisha dakika ya 89.