Chama afunguka bao lake, Luis ndani Msumbiji

Muktasari:

Katika mchezo dhidi ya Biashara United, Chama alifunga mabao mawili huku Miquissone akipiga pasi tatu zilizozaa mabao

Kiungo wa Simba, Clatous Chama amedai kuwa hakulenga jambo baya kwa kipa na beki wa Biashara United ambao aliwapiga chenga na kufunga bao la pili juzi na badala yake lengo lake lilikuwa ni kufunga tu.

 Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini, juzi Jumapili kuanzia saa 1.00 usiku, Simba waliibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 huku Chama akifunga mawili na kupiga pasi moja iliyozaa bao.

 Bao la pili ambalo Chama alifunga dakika ya 26 ndio lilikuwa gumzo kwani Chama mara baada ya kupokea pasi ya kupenyeza ya Luis Miquissone, aliwapiga chenga kwa wakati mmoja, beki na kipa wa Biashara United na kuujaza mpira huo kimiani, bao ambalo limekuwa gumzo.

 Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Chama ameandika kuwa hakulenga kuwaumiza wachezaji wa Biashara United kwa staili aliyotumia kufunga bao hilo.

 "Sikuwa najaribu kumuumiza yeyote. Nilikuwa najaribu kutengeneza urahisi kwangu kufunga na mguu ninaopendelea," ameandika Chama huku akiwaomba mashabiki kutembelea ukurasa wake wa You Tube ili kuona video ya bao hilo na nyinginezo.

 Wakati Chama akifunguka hayo, mwenzake Luis ni miongoni mwa wachezaji 34 walioitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Msumbiji kitakachokwenda kuweka kambi Ureno kuanzia Septemba 30 hadi Oktoba 16 kujiandaa na michezo ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2021.

 Luis ni miongoni mwa wachezaji tisa (9) wa nafasi ya ushambuliaji wanaounda kikosi hicho kilichosheheni nyota wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya Msumbiji.

 Katika kikosi hicho, kocha Luis Goncalves amelijumuisha pia jina la nahodha na mkongwe wa timu hiyo, Elias Gaspar Domingues 'Pelembe' (36) anayecheza nafasi ya winga wa kulia katika timu ya Bidvest Wits inayoshiriki Ligi Kuu  Afrika Kusini.

 Kikosi hicho cha Msumbiji kinaundwa na makipa Guirrugo (UD Songo), Frenque (CF Maputo), Victor (Costa do Sol) na Teixeira (ABB).

 Mabeki ni Infren (UD Songo), Fidel (ABB), Bheu (UD Songo), Zainadine (Maritimo), Sidique (UD Songo), Salomao (Costa do Sol), Mexer (Bordeaux), Bonera (Maritimo), Jeitoso (Ferroviario de Maputo), Reinildo (Lille), Edmilson (Cape Town FC) na Tununo (CF Maputo).

 Viungo ni Kambale (Baroka), Ricardo Mondlane (Sanjoanense), Nene (Costa do Sol), Xirasse (ABB), Kamo Kamo (Victoria de Setubal), Telinho (UD Songo), Domingues Elias 'Pelembe' (Bidvest Wits), Geny (Sporting Lisbon) na Kito (CF Maputo)

 Upande wa washambuliaji kuna Miquissone, Clesio (Zira FK), Nilton (Costa do Sol), Reginaldo (FC Kaysar), Ratifo (CfR Pforzheim), Lau King (UD Songo), Witi (Nacional) Amancio (Victoria de Setubal) na Gildo (Amora FC)