Chama; Mfalme mpya aliyeizima Mbabane

Monday December 10 2018

 

By Khatimu Naheka

MANZINI.PALE Eswatini dakika 45 za kwanza kati ya Simba na wenyeji Mbabane Swallows zilitosha kabisa kwa mashabiki wenyeji kutambua safari ya timu yao kusonga mbele ilikuwa imefutwa rasmi.

Wakati Simba ikienda mapumziko na hata ikirudi uwanjani mashabiki wa Swallows walikuwa wakimnyooshea kidole mtu mmoja anayeitwa Clatous Chama na kikwao walitamka maneno wakisema ‘Chama we ingothi’ wakimaanisha Chama ni hatari sana.

Clatous Chama ni nani?

“Ni mtu mwenye familia, Mkristo kwa imani. Pia, ni mchezaji mpira naamini hilo unalijua ni mtu anayeithamini familia yake na ajira yake ni soka. Juu ya yote anaijali sana familia yake na kipi kinatangulia kati ya mpira na familia? Familia kwanza. Kucheza mpira ni katika kuhakikisha familia yake inakwenda sawa,” Hayo ni maneno kutoka kwa Chama akijielezea alipofanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti.

Ujio wake Simba ulikuaje?

Akiendelea Chama anaelezea jinsi safari yake ya kutua Simba ilivyokuwa:”Ujio wangu kutoka Luaka Dynamo kuja Simba ilikuwa ni akili ya kuendelea mbele. Kwanza niwashukuru viongozi wa Simba na hata wachezaji na makocha. Unajua kabla ya safari yangu ya kutua hapa haijaanza, kufanya kazi hapa ilikuwa na mambo mengi ya sintofahamu.

“Ilikuwa ni safari ambayo ilisababishwa na mimi kuvunja mkataba na Lusaka Dynamo ambako huko nilikuwa nahodha wa timu kwahiyo haikuwa rahisi kwao kukubali kumpoteza lakini ndiyo maana nawashukuru viongozi kutokana na walijitahidi kutulia na kufuatilia suala langu mpaka nilipomalizana na Dynamo.

“Unajua wangeweza kuniambia ebu tumuache arudi kwao akamalizane na klabu yake lakini haikuwa hivyo, viongozi na makocha walikuwa sehemu ya kutafuta suluhu hiyo na mwisho wakafanikiwa na sasa nipo Simba.”

Sababu ya kuvunja mkataba

“Tatizo lilikuwa moja tu nilishindwa kulipwa mishahara yangu ya kama miezi kama mitano hivi, tukaamua mimi na meneja wangu tuvunje mkataba na wao hawakukubaliana na hilo lakini tulitumia sheria za Fifa kulimaliza hilo.”

Nani aliyemuona Simba?

“Siwezi kusema ni nani hasa aliyenileta hapa lakini ninachoweza kusema nilikuwa naijua Simba kabla. Niliwahi kuja hapa nikiwa na klabu yangu ya zamani ya Zesco wakati huo nikiwa kijana sana lakini ujio wangu sijajua rasmi ni nani aliyewasiliana na meneja wangu. Nakumbuka meneja alinifuata akaniambia Simba inahitaji mchezaji mwenye ubora kama wangu na ofa yao nikaijua na nikakubali kuja hapa.

Safari yake ya kutua Misri

Kama hufahamu, baada ya kuifikisha Zesco nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, Chama alitua Misri baada ya kununuliwa kwa fedha ndefu lakini hakuwa na msimu mzuri na kuamua kurudi Dynamo.

“Unajua safari yangu ya Misri ni historia ndefu wakati mwingine huwa sipendi kuiongelea nashukuru Mungu kuna kitu nilijifunza kupitia safari hiyo. Kuifanya kuwa fupi, safari yangu ya kwenda Misri haikuwa kitu kizuri kwa mashabiki wangu. Nashukuru Mungu sasa nimejifunza kitu na hata mashabiki wangu walinielewa na kusahau hilo ndio maana nikarudi nyuma na kujipanga upya na sasa maisha yamerudi.

Nafasi ipi anacheza uwanjani?

“Mimi ni mchezaji huru uwanjani lakini naweza kucheza nafasi yoyote yenye asili ya kushambulia ingawa mwenyewe napenda sana kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji wa pembeni nikitokea kushoto lakini kutokana na kocha wangu (Patrick Aussems) anataka kuniona nacheza nikiwa huru nikiwa na mpira na tukipoteza narudi katika majukumu mengine.

Anavyoiona Simba ya sasa

“Nafikiri tunakweda katika njia sahihi. Naona kuna mambo mengi mazuri yanakuja mbele na jambo zuri zaidi naona timu imekuwa na uwiano mzuri na tunaangalia mbele kuleta mafanikio hapa, kuleta furaha iliyokosekana kwa muda ingawa bado tuna safari ndefu mbele katika ligi ya nyumbani na hata Ligi ya Mabingwa tuzidi kuwa na umoja uliopo sasa.

Anakionaje kiwango chake sasa?

“Siwezi kujizungumzia lakini nafikiri naendelea kuwapa Simba kile kilichowafanya wanisajili katika klabu hii. Sijui wanaridhika au hawaridhiki kwa kiasi gani lakini binafsi naendelea kujituma kuisadia timu yangu.

Mastraika Simba anawaonaje?

“Nafikiri unafuatilia mechi na hata mazoezi yetu unaona tuko sawa. Tuna watu wanaojitambua kule mbele tunatengeneza nafasi za kuzitumia. Pia, hiyo ni dalili tuna watu bora katika timu bora. Hii ina maana mambo yanawiana vyema na hata kwa mabeki wetu nao wako sawa utaona ni jinsi gani haturuhusu mabao mengi.

Je, Aussems?

“Ni kocha mzuri sana. Namuelewa ni kocha ambaye anasimama katika misingi ya kazi yake anayejitoa kwa ajili ya timu lakini jambo zuri zaidi anatuamini wachezaji wake wote. Lakini pia tunamchukulia kama baba kutokana na kuna wakati mambo hayaendi sawa anatutuliza na kutufariji na baada ya muda unaona kweli mambo yanabadilika. Tunashukuru kuwa na kocha kama huyu na tutaendelea kumpa matunda ya kazi yake

Lwandamina kumleta Yanga?

“Kusema ule ukweli wakati baba yangu, napenda kumuita hivyo, Kocha George Lwandamina anakuja Yanga akili yangu yote nilidhani ningekuja Yanga kujiunga naye. Kwasababu kama ninavyosema alikuwa ni kama baba hana tofaui kubwa na Kocha Aussems na alipokuja nilidhani ningekuja Yanga kwa kuwa alishaniambia atanileta lakini baadaye mambo yakabadilika nikaenda kwingine kifupi nilikaribia kutua Yanga lakini sasa mambo hayako hivyo, nipo hapa nilipo sasa.

Simba itatetea ubingwa?

“Nafikiri tuko nafasi ya tatu sasa katika msimamo wa ligi na bado kuna mechi nyingi za kucheza na msimamo unaongozwa na Yanga. Nafikiri Yanga inafanya vizuri kuliko sisi lakini hii ni ligi na hata kama nasema Yanga inafanya vizuri sina maana tumeridhika na nafasi tuliyopo. Tunaangalia mbele lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu bila kujali uwezo wa Yanga na nina uhakika tutafanikiwa.

“Nafasi ya Simba kutetea ubingwa ni kubwa wala hilo mashabiki wasihofu kwa sasa ni suala la kutafuta uwiano mzuri katika kucheza Ligi ya Mabingwa na mechi za ligi tukifanikiwa hilo hakuna tatizo.

Tofauti ya Simba, anga na Azam

“Ninachokiona ligi ina ushindani sana lakini tatizo linakuja kila timu inayocheza na Simba inapambana kuhakikisha inaifunga.

“Lakini wakati mwingine nashangaa kuona timu hizohizo zikicheza na Yanga au Azam zinafungwa kirahisi s nafikiri hiyo ni changamoto kwetu tutaendelea kujituma kwa nguvu katika kila mchezo ili tuipe ushindi timu yetu.

Mabao mawili Caf

“Hii ni hatua nzuri kwangu kuanza kufunga katika mashindano ya Caf nikiwa na Simba. Nakumbuka hii ni mara ya pili kufunga mabao mawili katika mechi hizi. Naamnini huu ni mwanzo wa mambo mazuri zaidi unapofunga hali ya kujiamini inaongezeka zaidi.

Angekuwa nani?

“(Anacheka kidogo) sijui ningekuwa nani lakini bado najiona ningekuwa mtu wa mpira unajua baba yangu alikuwa mchezaji tena kiungo kama mimi. Nina kaka yangu wa kwanza, Henry Chama ni mchezaji alikuwa beki. Pia, kaka yangu Adrian Chama ni mchezaji pia yuko pale Green Buffaloes na hata mimi ni mchezaji.

Uwezo wake wa kumiliki mpira

“Unajua hiki ni kipaji ambacho Mungu amekupa kuna wakati unajikuta unavifanya vitu tu hakuna ninachopanga vinakuja tu. Ninachoshukuru vinaisaidia timu yangu vinginevyo nisingekuwa nafanya lakini pia kutokana na kuwa kati timu nzuri ubunifu zaidi unafanyika.

Anachotaka kufanya mbele zaidi

“Siwezi kusema mpira wangu nitamalizia hapa kama mchezaji wa Afrika. Ndoto yangu ni kucheza Ulaya lakini kwasasa nina mkataba na Simba najua natakiwa nifanye vizuri hapa kwanza hii ni timu kubwa pia, nitajituma ili hayo mengine yaje kirahisi.

Advertisement