Chama: Kishindo kinakuja

VIUNGO wa Simba, Clatous Chama na Larry Bwalya wanafahamu mashabiki wao wamekasirika na kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Prisons juzi na ili kuwapooza wameahidi ushindi mnono kesho dhidi ya Ruvu Shooting pale Uwanja wa Uhuru.

Matokeo hayo dhidi ya Prisons yameifanya Simba ishuke hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi nyuma ya Azam na Yanga jambo ambalo ni wazi limewakera mashabiki wao.

Hata hivyo, Chama na Bwalya ambao ni viungo washambuliaji wa timu hiyo, wameibuka na kuwataka mashabiki wao wajiandae kwa kishindo ambacho watakuja nacho katika mechi ya kesho dhidi ya Ruvu Shooting.

Chama, ambaye alikosa mechi iliyopita dhidi ya Prisons kwa ruhusa ya kwenda kwao kushughulikia hati yake ya kusafiria, ametamba kuwa watakuja kivingine baada ya kupoteza mchezo uliopita.

“Urejeo wetu baada ya kupoteza mechi iliyopita utakuwa ni wa kihistoria. Sisi ni Simba,” aliandika Chama katika ukurasa wake wa Twitter.

Hii itakuwa ni ahadi ya pili kutolewa na Chama msimu huu pindi Simba inapokuwa na mwenendo usioridhisha na mara ya kwanza alifanya hivyo baada ya Simba kucheza mechi mbili za ugenini dhidi ya Ihefu na Mtibwa Sugar na kuvuna pointi nne.

Kabla ya mchezo uliofuata dhidi ya Biashara United, Chama aliwaahidi mashabiki wa Simba kuwa watacheza soka la kuvutia na pia kuibuka na ushindi mnono.

“Msimu ndio kwanza umeanza na tunahitaji rekodi nzuri hasa tukiwa nyumbani. Tunatakiwa kushinda kuanzia mabao mawili hadi matatu kwa kila mechi.

“Tutaifanyia kazi na nina uhakika tutapata matokeo mazuri. Tunafahamu Biashara wana rekodi nzuri ya safu ya ulinzi, mechi itakuwa ngumu lakini tunajua nini cha kufanya,” alinukuliwa Chama.

Ahadi hiyo ya Chama ilikuja kufanyiwa kazi kwa vitendo na wachezaji wa Simba kwani, walionyesha kiwango cha hali ya juu huku wakiibuka na ushindi wa mabao 4-0 na mawili yakipachikwa na Chama.

Kama ilivyo kwa Chama, Bwalya naye alisema wanahitaji kushinda shisi ya Ruvu.

“Sio matokeo tuliyoyategemea lakini, tutarudi kwa nguvu na imara zaidi,” alisema.

Naye kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema kwa sasa wanaitazama zaidi mechi ya Ruvu na hawaifikirii iliyopita.

“Hii ni ligi, baada ya mechi moja unajiandaa na nyingine,” alisema Sven.