Chama, Kagere wanavyotingisha mastaa Ligi ya Mabingwa Afrika

Muktasari:

Nyota tegemeo wa Simba katika safu ya ushambuliaji, Meddie Kagere, anatarajiwa kutumia uzoefu wake katika mashindano haya kuongeza makali katika mbio za kuwania tuzo ya kiatu cha mfungaji bora.

HUKO kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kumezidi kunoga unaambiwa. Droo ya robo fainali ndio imeshafanyika na mabingwa wa kutandaza soka Tanzania Bara, Simba Imepangwa kumenyana na TP Mazembe ya DR Congo kwenye hatua hiyo ya nane bora. Mambo ni moto.

Hata hivyo, utamu huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika una mambo mengi, ikiwamo ile vita ya mchakamchaka wa kuwania Kiatu cha Dhahabu na kuna mastaa kibao wanatoana jasho kwenye kuiwania tuzo hiyo binafsi yenye hadhi kubwa kwa mchezaji husika. Hii hapa ndiyo ile orodha ya mastaa wanaochuana jino kwa jino katika kuifukuzia tuzo hiyo ya mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

NAHIRI (4) - CASABLANCA

Anacheza katika timu inayotazamwa na wengi kutokana na ubora ilionao na ana angalau michezo miwili (nyumbani na ugenini) katika hatua ya robo fainali inayompa fursa ya kuongeza akaunti yake ya mabao. Mabao yake manne aliyafunga katika mechi nne tofauti, lakini hilo halimaanishi kwamba hawezi kufunga zaidi ya bao moja kwenye mechi moja.

Anaweza kutwaa tuzo ya mfungaji bora kama ataongeza juhudi katika mechi zinazoendelea, ambapo timu yake imetinga robo fainali.

MULEKA (4) - TP MAZEMBE

Anatarajiwa kukutana na ukuta wa Simba katika mechi mbili za robo fainali. Kama Simba itamdhibiti yeye na wenzake Dar es Salaam Aprili 6 basi ndoto zake za kutwaa tuzo ya kiatu cha dhahabu zitamalizikia Lubumbashi, DR Congo katika mchezo wa marudiano.

Katika mchezo mmoja alifunga mara mbili kabla ya kutupia bao moja moja katika mechi zilizofuata, jambo linaloleta picha ni mchezaji anayeweza kufanya makubwa sana katika mbio za kuwania tuzo ya Kiatu cha Dhahabu.

MPUTU (4) - MAZEMBE

Ni mchezaji wa pili kutoka katika timu moja kuwa na idadi sawa ya mabao akiwa ametupia kambani mara nne na kuisaidia timu yake kutinga robo-fainali.

Na baada ya droo kuchezeshwa na kujikuta meza moja dhidi ya Simba, Mputu atajaribu kuisaidia Mazembe kurudia mafanikio yake ya mwaka 2012 katika michuano hiyo ilipoifunga Simba kwa jumla ya mabao 6-3.

Hata hivyo, Simba ilicheza mechi dhidi ya Wydad Cassablanka baada ya Mazembe kuenguliwa mashindanoni kwa kumchezesha Mchezaji Besela Bukungu kimakosa.

Katika mechi sita za hatua ya makundi msimu huu, Mazembe imefunga jumla ya mabao 13, yakiwamo 8-0 ya mechi yao moja ya mwisho dhidi ya Club Africain ya Tunisia.

ZWANE (5) - MAMELODI SUNDOWN

Kiungo huyo raia wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 29, ni kati ya nyota waliong’ara katika Ligi ya Mabingwa msimu huu akitupia mabao matano. Mamelodu Sundown itaikabili Al Ahly, ikianzia nyumbani Afrika Kusini na kumalizia ugenini Misri.

CHAMA (5) - SIMBA

Anacheza nafasi ya kiungo cha ushambuliaji na ni mchezaji ambaye katika msimu wake wa kwanza tu tangu ajiunge na Simba ametokea kuwa kipenzi cha mashabiki.

Alinogesha ‘keki’ ya kupendwa kwake baada ya kufunga bao muhimu la ushindi katika dakika za lala salama dhidi ya AS Vita kwenye Uwanja wa Taifa na kuwapeleka Wekundu wa Msimbazi katika hatua ya robo fainali.

Ndiye mchezaji pekee wa Simba aliyefunga mabao mawili ugenini msimu huu baada ya kufanya hivyo katika mechi ya hatua ya awali ya kuwania kufuzu kwa hatua ya makundi dhidi ya Mbabane Swallows, ambayo Wekundu wa Msimbazi walishinda 4-1 nyumbani na 4-0 ugenini.

KAGERE (6) - SIMBA

Nyota tegemeo wa Simba katika safu ya ushambuliaji, Kagere, anatarajiwa kutumia uzoefu wake katika mashindano haya kuongeza makali katika mbio za kuwania tuzo ya kiatu cha mfungaji bora.

Kagere ana angalau dakika 180 za kumfikia kinara wa sasa wa mabao Moataz Al-Mehdi aliyetupia mabao saba. Anaweza pia kumpita Al-Mehdi,

ambaye timu yake ya Al Nasry ilishatolewa katika hatua ya makundi.

MOATAZ AL-MEHDI (7) - AL NASRY

Ndiye kinara wa mabao Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini timu yake imeshatolewa. Al Mehdi atawaombea wapinzani wake katika mbio hizo wasiifikie idadi ya mabao aliyofunga ili aweze kutwaa kiatu cha dhahabu. Katika mechi tatu alitupia maba mawili-mawili na bao la saba alitupia kwenye mchezo wake ambao timu yake ilishindwa kuingia hatua ya m robo fainali.