Chalenji yaitibulia Yanga kwa Fei Toto

Muktasari:


Zanzibar Heroes ilishika nafasi ya pili katika mashindano ya Chalenji yaliyofanyika Kenya mwaka jana.

VIUNGO wa Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto', Abdulaziz Makame na Mohamed Issa 'Banka' hawakuungana na wenzao katika mazoezi ya kujiandaa na Alliance Ijumaa.
Viungo hao wamekosa mazoezi ya leo na jana kutokana na kwenda Zanzibar kujiunga na timu yao ya Taifa 'Zanzibar Herros' kwa ajili ya mashindano ya Chalenji yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli alisema Makame na Fei wamepewa ruhusa maalumu na uongozi.
"Bodi ya ligi imetubadilishia ratiba tukiwa tayari tumeshatoa mapumziko kwa wachezaji na Makame na Fei Toto tumeshindwa kuwarudisha kwa kuwa, wamejiunga na kambi ya Zanzibar Heroes moja kwa moja."
Awali, ratiba ilionyesha hatutakuwa na mchezo ligi hadi Januari 4 dhidi ya Simba, lakini sasa tumepewa ratiba nyingine," alisema Bumbuli.
Bumbuli aliongeza, hivyo wachezaji hao hawatakuwa sehemu ya kikosi kinachotarajia kusafiri alfajiri ya kesho kwenda Mwanza.