VIDEO: Cech, Van Persie wawaongoza mastaa kibao kutundika daruga

Muktasari:

  •  Mbali na umri kuwatupa mkono baadhi ya mstaa barani Ulaya, kuna wengine wamekuwa wakiwahi kutundika daruga kutokana na majeraha sugu ambayo yamekuwa yakiwafanya kuwa nje ya uwanja mara kwa mara.

 

WAPENZI mbalimbali wa soka la Ulaya, macho na masikio yao wanayaelekeza kwenye dirisha la usajili litakalofunguliwa wiki chache zijazo  lakini ni vema tutambua kuwa kuna mastaa ambao wamezipa mkono wa kwakheri klabu zao.

Miongoni mwa mastaa hao ni gwiji  wa Chelsea, Petr Cech ambaye amemalizia soka lake kwa washika mitutu wa London  na Robin Van Persie ambaye aliwahi kuichezea Manchester United kwa mafanikio.

Hii ni orodha ya mstaa  watano barani Ulaya ambao wametangaza kutundika daruga msimu huu wa 2018/19.

 Robin van Persie

Mai 12  mwaka huu, Van Persie alicheza mchezo wake wa mwisho ambao walipoteza akiichezea Feyenoord kwa mabao 2-0 dhidi ya ADO Den Haag, Mshindi huyo wa Ligi Kuu England msimu wa 2012/13 akiwa na United, aliagwa kwa heshima  dakika ya 93 ambapo alitolewa na nafasi  yake  akaingia Dylan Vente.

Petr Cech

Cech, 36, mwenye rekodi ya kutoruhusu nyavu zake kuguswa kwenye mechi 202 kati ya michezo 443, aliyocheza Ligi Kuu England ‘EPL’, ataangwa rasmi kwenye mchezo wa fainali ya Europa Ligi dhidi ya timu yake ya zamani ya Chelsea, Mei 29.

Andrea Barzagli

Aprili 13, baada ya kupata nafasi ya kucheza, Barzagli, 38,  kwenye mchezo wa Ligi Kuu Italia ‘Serie A’ ambao Juventus ilipoteza kwa mabao 2-1 mbele ya  SPAL, beki huyo aliyeshinda mataji nane akiwa na vibibi kizee hivyo vya Turin, alisema atastaafu mwishoni mwa msimu huu.

Yossi Benayoun

Mchezaji wa zamani wa West Ham, Liverpool, Chelsea, Arsenal na QPR, Yossi Benayoun, 39,  kwenye mchezo wake wa mwisho akiwa na Beitar Jerusalem alionekana kuwa na watoto wake watano ambapo wote kwa pamoja walikwa wakiwapungia mkono wa kwakheri mashabiki wa timu hiyo.

Xavi

Nyota wa zamani wa Barcelona, Xavi ,38, ambaye alikuwa akiichezea Al Sadd ya Qatar naye ametangaza kustaafu na badala yake atageukiwa majukumu ya ukocha ambayo anatarajiwa kuyaanza ndani ya mwezi huu, Mei.

Nyota wengine ambao na wenyewe wametangaza kustaafu msimu huu ni pamoja na Sergio Pellissier ,40, wa Chievo, John O’Shea,38, (Reading),  Bruno, 38, (Brighton & Hove Albion) na Matty Taylor ,29, wa  Bristol City.