Carragher adai viungo wa Liverpool vimeo

Muktasari:

Carragher anaamini Liverpool kushindwa kupenya ngome ya kikosi cha Diego Simeone imetokana na kukosekana kwa viungo mafupi na wabunifu kwenye kikosi hicho cha Klopp.

LIVERPOOL, ENGLAND. Beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher amesema viungo wa timu hiyo walikosa ubunifu kwenye mchezo dhidi ya Atletico Madrid huku akikiri kwamba miamba hiyo ya La Liga ilistahili ushindi kwenye mchezo wao wa kwanza wa mtoano hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Liverpool, ambao ni mabingwa watetezi walikumbana na kichapo cha bao 1-0 katika mchezo huo uliofanyika Hispania juzi Jumanne watasubiri kuona kama watageuza kibao kwenye mechi ya marudiano itakayopigwa Anfield mwezi ujao.

Chama hilo la Jurgen Klopp lilichapwa bao la mapema sana lililofungwa na Saul Niguez baada ya kuuwahi mpira uliokuwa ukizagaazagaa kwenye eneo la penalti.

Liverpool walimiliki mpira sehemu kubwa ya mchezo, lakini walishindwa kupiga shuti hata moja golini kutokana na beki ngumu ya Atletico iliyoiwekea ngumu fowadi ya wababe hao wa Anfield.

Carragher anaamini Liverpool kushindwa kupenya ngome ya kikosi cha Diego Simeone imetokana na kukosekana kwa viungo mafupi na wabunifu kwenye kikosi hicho cha Klopp.

"Ulikuwa usiku wa kuumiza kwa Liverpool," alisema Carragher.

"Tufahamu namna Atletico wanavyocheza, Jurgen Klopp anafahamu pia. Lakini, ukweli ni kwamba huwezi kushinda mechi kama hizi kama utakuwa wa kwanza kuruhusu bao, hasa kwa bao lile walilofungwa. Liverpool walikosa ubunifu kwenye sehemu ya kiungo na siku zote hilo limekuwa tatizo kwao."