SALUTI : Carragher ,Ramsey wanyoosha mikono kwa Aubameyang

Muktasari:

  • Aubameyang juzi Jumapili alifanya shoo ya kibabe dhidi ya Tottenham baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-2 wa Arsenal dhidi ya watani hao wa London Kaskazini na Carragher amekiri Aubameyang ambaye amefikisha mabao 10 ya Ligi Kuu msimu huu ni tishio.

LONDON, ENGLAND.TATIZO jingine limeingia ka tika Ligi Kuu ya England. Pierre-Emerick Aubameyang. Mtu mmoja anaamini staa huyu wa Gabon anaweza kuwa tatizo kwa mabeki wa timu pinzani kuliko Sergio Aguero au Harry Kane.

Jamie Carragher, staa wa zamani wa Liverpool ni mchambuzi mahiri wa soka England amedai nyota huyo anatisha tangu atinge katika Ligi Kuu ya England ingawa watu wengine wamekuwa wakimchukulia poa.

Aubameyang juzi Jumapili alifanya shoo ya kibabe dhidi ya Tottenham baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-2 wa Arsenal dhidi ya watani hao wa London Kaskazini na Carragher amekiri Aubameyang ambaye amefikisha mabao 10 ya Ligi Kuu msimu huu ni tishio.

“Yule jamaa anaweza kuwa Supastaa wa Ligi Kuu. Hatumuongelei sana. Mara zote tumekuwa tukiwafikiria zaidi kina Kane na Aguero lakini Aubameyang amejitokeza katika anga za Ligi Kuu. Tangu alipofika Januari katika siku za mwisho za zama za Wenger, uwezo wake wa kufunga mabao ni mzuri kama mchezaji mwingine yeyote,” alisema Carragher.

“Siku zote nimekuwa nikimuangalia (Alexandre) Lacazette na kudhani ni mchezaji mzuri, lakini kila ninapomuangalia huyu jamaa (Aubameyang) nadhani ni mzuri sana,” aliongeza Carragher.

Naye staa wa kimataifa wa Wales wa Arsenal, Aaron Ramsey ambaye aliingia katika kipindi cha pili katika mchezo wa juzi na kupika mabao mawili alidai Aubameyang ni mshambuliaji hatari na anamkumbusha staa wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry.

“Hauwezi kuamini anayofanya lakini amekuwa akifanya hivyo kila wakati. Mara nyingi anaupeleka mpira kirahisi katika kona za nyavu, lakini pia ana kasi. Ananikumbusha Thierry Henry (staa wa zamani wa Arsenal),” alisema Ramsey.

Staa huyo aliyenunuliwa kwa dau la Pauni 58 milioni kutokea Borussia Dortmund katika dirisha dogo la Januari mwaka huu amekuwa akifunga mabao mengi tangu alipofunga bao lake la kwanza katika mechi yake ya kwanza tu klabuni dhidi ya Everton Februari.

Kwa sasa ana mabao 20 katika mechi zake 27 tu za Ligi Kuu ya England tangu awasili. Hakuna mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika ligi hiyo tangu yeye awasili. Ni mabao matatu zaidi ya Kane na manane zaidi ya Aguero.

Staa huyo wa Gabon pia ametumia dakika chache zaidi kufunga mabao hayo kuliko wapinzani wake. Kila bao lake lina wastani wa kufungwa baada ya dakika 104 kulinganisha na wastani wa kila bao lililofungwa na Aguero aliyetumia dakika 110 wakati Mohamed Salah wa Liverpool ametumia dakika 113. Mabao 17 ya Kane kuanzia Januari mpaka sasa yamekuja kila baadaya dakika 135.

Aubameyang pia mara nyingi amekuwa akichezeshwa nje ya nafasi yake na kocha wa sasa, Unai Emery. Licha ya kufunga mabao hayo lakini mechi saba kati ya 13 amecheza akitokea upande wa kushoto huku Lacazette akitokea kati.

Wakati huohuo shabiki mmoja wa Tottenham anashikiliwa na polisi baada ya kumtupia ganda la ndizi Aubameyang mara baada ya kufunga bao moja kati ya mawili aliyofunga juzi Jumapili. FA ya England pia imefungua uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Kamera za CCTV zilimnasa shabiki huyo kabla ya polisi kumtia ndani lakini baadaye inadaiwa jumla ya mashabiki saba walitiwa ndani huku sita kati yao wakiwa na makosa mbalimbali. Wawili kati ya hao ni mashabiki wa Arsenal ambao waliwasha moto uwanjani.