Cape Verde yaipania Taifa Stars

Muktasari:

Timu mbili kutoka kila kundi zinafuzu moja kwa moja kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon.

Praia, Cape Verde. Cape Verde itakuwa wenyeji wa Tanzania katika mchezo wa Kundi L wa kusaka kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019.

Mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Cabo Verde jijini Praia leo Ijumaa saa 2:00 usiku.

Cape Verde ‘Blue Sharks’ walilazimishwa sare 1-1 na Lesotho katika mchezo wake wa ugenini iliyocheza mwezi uliopita.

Sare hiyo imeifanya Cape Verde kuendeleza rekodi yake ya kutopoteza mechi tatu zilizopita za mashindano yote ikiwa imeshinda mechi mbili na sare moja.

Timu hiyo wa Afrika Magharibi itakuwa inataka kuendeleza rekodi yake ya kutofungwa wakati watakapoikabili timu isiyotabilika ya Tanzania.

Wakati Tanzania inakwenda katika mchezo huo ikiwa imelazimisha suluhu na Uganda katika mchezo wao uliopita.

Matokeo hayo yanaifanya Taifa Stars kuweka rekodi ya kutofungwa katika michezo miwili iliyopita ya mashindano yote.

Miamba hiyo ya Afrika Mashariki inahitaji kushinda dhidi ya Cape Verde iliyokuwa katika kiwango bora ili kujiweka vizuri katika kundi hilo.