VIDEO: Cannavaro aagwa kwa kiroba cha mchele

Sunday August 12 2018

 

By GODFREY KAHANGO, MBEYA

MASHABIKI wa Yanga Mbeya mjini wamemzawadia kilo 40 za mchele mchezaji wao, Nadir Haroub Cannavaro’ ikiwa ni sehemu ya kutoa heshima na kutambua mchango wake wa kuitumikia klabu hiyo hadi alipoamua kustaafu soka.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Msaidizi wa mashabiki wa Yanga Mbeya Mjini, Rajab Mrisho alisema wanatambua mchango mkubwa aliouonesha mchezaji wao katika kuitumikia Yanga hivyo wao wameona bora watoe zawadi kidogo ya mchele ambao atakabidhiwa leo Jumapili mjini Morogoro atapoagwa.

Yanga watacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mawenzi Market mechi ambayo wataitumia kumuaga rasmi Cannavaro ambaye alikuwa nahodha wa Yanga kwa zaidi ya miaka 10.

“Kwa heshima ya pekee kabisa, sisi mashabiki wa Yanga Mbeya mjini tumeamua kumuaga Canavaro kwa kumpatia zawadi ya mchele, ambao utamfikia kesho (leo) ameitumikia timu yetu kwa mapenzi mema kabisa,” alisema Mrisho.

Akizungumzia namna walivyojipanga katika msimu ujao kuipa ‘sapoti’ timu yao, Mrisho alisema wapo vizuri na sasa wanaendelea kujipanga vilivyo kuhakikisha wanaipokoea vizuri timu yao kila itakapokuwa inakanyanga ardhi ya Mbeya.

“Kwa sasa hatuna papara lakini tupo vizuri na tunajipanga vyema kabisa, tutahakikisha timu yetu inaondoka na pointi tatu kila inapocheza mpira hapa Mbeya na hili tumepania haswaa.”

Advertisement