Campbell kurudiana na Mendy

London, England. Bondia Luke Campbell kutoka Uingereza, amepata nafasi ya kuuthibitishia ulimwengu madai yake kuwa alipoteza pambano dhidi ya Yvan Mendy kwa kudhulimiwa.

Campbell alishindwa kwa pointi katika pambano hilo lililofanyika mwaka 2015 lakini  alipinga kushindwa pambano hilo akidai kuwa yeye ndiye aliyestahili kushinda pambano hilo dhidi ya Mendy.

Hilo lilikuwa pambano la kwanza kwake kupoteza tangu ajitose kwenye ngumi za kulipwa.

Campbell bingwa wa Olimpiki uzani wa Light, atapanda ulingoni Septemba 22 mwaka huu kuzipiga katika pambano la kuwania ubingwa wa WBC kwenye uwanja wa Wembley.

Mendy, mwenye miaka 33, ndiye bondia anayeshikilia nafasi ya kwanza kwa ubora uzani wa Light anayetambuliwa na WBC na hajawahi kupoteza pambano lolote tangu mwaka 2015.

Pambano hilo la Campbell, mwenye miaka 30, litakuwa la utangulizi kabla ya pambano la ubingwa wa Dunia uzito wa juu wa WBC lkati ya Anthony Joshua wa Uingereza na Alexander Povetkin wa Russia.