Cameroon yaitisha Guinea

Muktasari:

Akizungumza jana, Kocha Camara aliwaambia waandishi wa habari, Cameroon wanaweza kunufaika na maumbile ya wachezaji wao lakini wao wanatafuta namna ya kuhakikisha wanawadhibiti.

PAZIA la Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana (Afcon) U17, limefunguliwa jana Jumapili, lakini unaambiwa saa chache kabla ya kuumana na Cameroon, timu ya Guinea imekiri kwamba hofu yao ni mabavu ambao wapinzani wao wanayatumia kwenye soka lao.

Kocha Mkuu wa Guinea, Mohammed Camara ni kama ameingia mchecheto juu ya maumbile ya wapinzani wao na kudai mechi yao ya leo Jumatatu kwenye Uwanja wa Azam Complex, utakuwa mgumu kwao.

Akizungumza jana, Kocha Camara aliwaambia waandishi wa habari, Cameroon wanaweza kunufaika na maumbile ya wachezaji wao lakini wao wanatafuta namna ya kuhakikisha wanawadhibiti.

“Faida kubwa ambayo wenzetu wanaingia nayo kwenye mchezo wa kesho (leo) ni kuwa na wachezaji wenye maumbile makubwa ambao haitokuwa kaI rahisi kukabiliana nayo. Lakini jambo ambalo litakuwa faida kwetu pindi tunapokabiliana na timu ya aina hiyo ni kucheza soka la ufundi na mbinu,” alisema Camara.