Cameroon yaanza vyema

Muktasari:

  • Mpaka Mwanaspoti linakwenda mitamboni Cameroon walikuwa wanaongoza kundi wakiwa na pointi tatu kundi B, wakati pambano la Morocco dhidi ya Senegal likiwa linaendelea katika Uwanja huo huo.

KIKOSI cha timu ya Taifa ya Cameroon kimeanza vizuri mashindano ya Mataifa Afrika Afcon ( U 17), baada ya kuwafunga Guinea mabao 2-0, katika mchezo wa kwanza wa timu zote mbili kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Mabao ya Cameroon yalifungwa na Steve Mvoue dakika ya 24, kabla ya Leonel Djouffo kufunga bao la ushindi dakika ya 72, na kuifanya timu hiyo kuondoka na pointi tatu.

Guinea waliweza kupiga mashuti manane huku lililolenga lango likiwa ni moja, wakati Cameroon walipiga saba na ambayo yalilenga lango la wapinzani wao yalikuwa manne, katika kupiga pasi ndani ya dakika 90, Guinea walikuwa bora kwani zao zilifika 305, wakati Cameroon 261.

Katika kumiliki mpira Guinea walipata asilimia 55, wakati Cameroon walikuwa na asilimia 45, Cameroon pia waliweka rekodi katika mchezo huo kwa wachezaji wake watano kupata kadi za njano huku Guinea hawakupata.

Mpaka Mwanaspoti linakwenda mitamboni Cameroon walikuwa wanaongoza kundi wakiwa na pointi tatu kundi B, wakati pambano la Morocco dhidi ya Senegal likiwa linaendelea katika Uwanja huo huo.

Leo Jumanne kutakuwa na mapumziko ya michuano hiyo lakini kesho Aprili 17, Serengeti Boys wenyeji watakuwa Uwanja wa Taifa saa 01: 00, usiku kucheza mchezo wa pili dhidi ya Uganda ambao nao walipoteza mechi ya kwanza na timu ambayo itafungwa katika mechi hii itakuwa imeaaga mashindano.

Mchezo mwingine utakuwa saa 10:00 ambao utawakutanisha Angola dhidi ya Nigeria na timu itayoshinda kati yao itakuwa imefuzu nusu fainali na kupata nafasi ya kucheza kombe la dunia kwani zote zilishinda mechi zao za kwanza.