Camavinga: Sifui jezi ya Ronaldo

Muktasari:

Makinda wengi duniani wamekuwa wakitamani kucheza sambamba na Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Paris, Ufaransa. UNAWEZA usiamini lakini ndio mambo yalivyo. Mchezo wa Uefa Nations League kati ya Ufaransa na Ureno umedhihirisha umaarufu wa Cristiano Ronaldo.

Katika mchezo huo ambao umeisha kwa sare, Ronaldo akiwa na chama lake ambao ndio mabingwa wa Ulaya, walikutana na Mabingwa wa Dunia, Ufaransa ambapo baada ya mchezo kumalizika kila mtu stori ikawa ni Ronaldo.

Iko hivi. Baada ya mchezo huo mastaa wa Ufarasa wakiongozwa na Klyian Mbappe kila mmoja alivamia kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii na kuelezea furaha ya kukutana na supastaa huyo anayekipiga Juventus ya Italia na mshindi wa mara tano wa tuzo ya Balon d'Or.

Hata hivyo, furaha zaidi ikawa kwa kiungo fundi mwenye kipaji cha soka, Eduardo Camavinga ambaye alipata bahati ya kupewa jezi na Ronaldo.

Camavinga, ambaye anapewa nafasi kubwa kutua Manchester United kwenda kumbadili Paul Pogba, amefichua kuwa kamwe hataifua jezi hiyo aliyopewa na Ronaldo na kwamba, itabaki kuwa ukumbusho kwake.

“Sitaifua kabisa,” Camavinga aliandika kwenye ukurasa wake huku akiwa ameambatinisha na picha ya jezi yenye jina na namba ya Ronaldo ambayo aliiva kwenye mchezo huo.

Camavinga,17, anayecheza kwenye kikosi cha Rennes ya Ufaransa, amekuwa gumzo kwenye michuano hiyo ya Ulaya kutokana na kuonyesha kiwango cha juu.

Pia, alifunga bao matata kwenye ushindi wa mabao 7-1 uliopata Ufaransa dhidi ya Ukraine. Hata hivyo, Manchester United italazimika kupambana kama Real Madrid wataonyesha nia ya kuwania saini yake kwani, mwenyewe anatamani kufuata nyayo za Ronaldo pale Santiago Bernabeu.