Caf kuamua hatima ya Simba leo

Muktasari:


Msimu wa 2018/2019, Simba ilitinga hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba leo watajua rasmi kalenda ya mashindano yaliyo mbele yao mara baada ya kikao cha kamati ya utendaji ya  Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Caf, kikao hicho cha kamati ya utendaji kitafanyika kwa njia ya mtandao wa video kuanzia saa 2.00 usiku na ndicho kitatoa hatima ya mashindano mbalimbali yanayosimamiwa na shirikisho hilo.
Baada ya mashindano mbalimbali kusimama katika kipindi cha zaidi ya miezi mitatu kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona, kikao cha leo kitatoa uamuzi na kupanga kalenda ya kuendelea kwa mashindano hayo na yale ambayo bado hayajafanyika.
Kikao cha leo kitajadili na kupanga kalenda ya mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021 na pia muda wa mashindano hayo kuchezwa hapo mwakani.
Pia kitatoa hatima ya mashindano ya Ligi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu na msimu ujao ambao Tanzania itawakilishwa na Simba.
Lakini pia pia kitatoa kalenda mpya ya mashindano ya Matifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ndani (Chan) sambamba na yale ya Afrika kwa Wanawake (Awcon) ambayo yalipaswa kuchezwa mwaka huu.
Kana kwamba haitoshi, kikao hicho pia kitajadili suala la kuanzishwa kwa ligi ya Mabingwa Afrika upande wa soka la wanawake ambalo linaonekana kushika kasi katika miaka ya hivi karibuni.
Kikao hicho kitaongozwa na Rais wa Caf, Ahmad Ahmad ambaye muda wake wa kuongoza shirikisho hilo unaelekea ukingoni.
Simba imekata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao baada ya kutangazwa rasmi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu msimu huu wakiwa wamekusanya jumla ya pointi 79 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote kwenye ligi hiyo.