CHRISS MUGALU: Nisipofunga huwa nakosa raha kabisa

MSIMU uliopita Simba walimaliza Ligi Kuu Bara wakiwa na mabao 78 ya kufunga ambayo yalichagizwa na kasi ya mastraika wawili - nahodha John Bocco na Meddie Kagere ambaye aliibuka kuwa mfungaji bora akiwa na mabao 22.

Msimu huu safu hiyo ya ushambuliaji imeongezwa mastraika wawili ambao ni Charles Ilanfya aliyeitumikia timu hiyo katika mechi tatu za kirafiki na kufunga mabao matatu pamoja na Chriss Mugalu aliyecheza michezo sita katika mashindano yote na kufunga mabao saba.

Mwanaspoti lilizumgumza na Mugalu ambaye alieleza kwa mara ya kwanza kupitia gazeti hili baadhi ya malengo ambayo amejiwekea msimu huu sambamba na kikosi cha Simba anavyokiona pamoja na mambo mengi.

USHINDANI WA MASTRAIKA

Mugalu anasema kabla ya kuja Tanzania wakati Simba walipomfuata kuonyesha nia ya kumhitaji, alitenga muda wa kutosha kuifuatilia timu hiyo hasa katika nafasi ambayo anacheza na kubaini kuna washambuliaji wenye uwezo wa kufunga mabao katika mechi mfululizo.

“John Bocco ndiye kapteni wangu, namheshimu kwa hilo, lakini hata makubwa ambayo ameyafanya katika soka hili la Tanzania, hivyo hivyohivyo kwa Meddie Kagere na Charles Ilanfya wote wana uwezo wa kutimiza majukumu yao ya kufunga mabao mara kwa mara,” anasema Mugalu.

“Ushindani uliopo kati yetu mastraika wa Simba ndio unaongeza morali na kasi ya kila mmoja ambaye anapata nafasi ya kucheza kutaka kufanya vitu bora ili aendelee kuaminiwa.”

Akizungumzia ushindani kikosini, Mugalu anasema: “Kuhusu ushindani ambavyo nimeuona kwangu wala si tatizo, kwani hakuna mchezaji ambaye anaweza kufanya bila kukutana na changamoto za kuwania nafasi ya kucheza, na katika timu zote ambazo nimepita kucheza soka nimewahi kukutana na changamoto kama hii.”

REKODI YA MMACHINGA

Katika Ligi Kuu Bara mchezaji ambaye amefunga mabao mengi na kuweka rekodi hiyo muda wote ni Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ ambaye mwaka 1999 alimaliza msimu akiwa na mabao 26 ambayo mpaka sasa hakuna straika aliyeifikia wala kuivunja.

Rekodi nyingine ambayo ipo hapa nchini mchezaji wa kigeni aliyewahi kufunga mabao mengi ni Kagere katika msimu wa 2018-19 alipomaliza akiwa amefunga mabao 23.

Hata hivyo, Mugalu anasema kama mshambuliaji majukumu yake ya kwanza ni kuhakikisha anatoa mchango kwa timu ambao ni kufunga mara kwa mara katika kila nafasi ya kufanya hivyo, ambayo atakuwa akipata kwenye mechi mbalimbali.

“Nashukuru nimeanza msimu vizuri katika mechi zote ambazo nimecheza, nimefanikiwa kufunga mabao jambo ambalo naamini mpaka kufika mwisho wa ligi kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu nitafanikiwa kumaliza na mabao mengi zaidi,” anasema.

“Sikuwa nafahamu kama kuna rekodi hiyo mfungaji bora wa ligi muda wote kumaliza na mabao 26, nitazidi kupambana kadri ambavyo naweza ili kuisadia timu na kufunga mabao mengi zaidi kama malengo yangu yalivyo,” anasema Mugalu.

Atoboa SIRI

Mugalu anasema huwa anajiwekea malengo ya kila mechi kufunga na kama ikitokea ameshindwa kufanya hivyo huumia moyoni, jambo ambalo linamfanya kukosa amani mpaka hapo atakapokuja kufunga katika mchezo ambao unafuata.

“Nisipofunga huwa nakosa raha kabisa ila kama ikitokea nimefunga moyo wangu unakuwa na amani jambo ambalo linanisababishia kuwa na hamu ya kufunga mabao mengine zaidi, ndio maana najiona naweza kumaliza msimu nikiwa na mabao mengi zaidi ya wakati huu.”

MABAO YOTE

Simba msimu huu ina mashindano manne mbele yao ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC), Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Mapinduzi.

Mugalu anasema hawezi kufahamu katika mashindano yote hayo ambayo Simba watashiriki msimu huu atamaliza akiwa na mabao mangapi, lakini malengo yake ni kufunga mabao mengi zaidi kadri iwezekanavyo.

“Ni ngumu kufahamu katika mashindano haya yote nitamaliza msimu nikiwa nimefunga (mabao) mangapi, ambalo naweza kueleza nitafunga mabao mengi msimu huu kwa mipango ya Mungu, hilo linawezekana bila shaka yoyote,” anasema.

TIMU ALIVYOIONA

Kuhusu Simba, Mugalu anasema: “Kwa ambavyo nimeiona Simba msimu huu ina kikosi ambacho kina malengo ya kufanya vizuri katika mashindano yote ambayo tunashiriki na kila mchezaji anatakiwa kujitambua ili kutimiza majukumu yake muda wote anapokuwa uwanjani.

“Simba imejengeka na ina wachezaji wenye uwezo jambo ambalo linamesababisha katika kila nafasi moja kuwa na wachezaji si chini ya wawili ambao wanashindana kwelikweli ili mmoja kati ya hao aweze kupata nafasi ya kucheza mbele ya mwenzake,” anasema Mugalu amesajiliwa na Simba kwa mkataba wa miaka miwili.

KUCHEZA NA BOCCO KAGERE

Mugalu anasema mbali ya ushindani ambao upo katika kikosi chao, lakini huwa anafurahi kucheza kwa pamoja na mastraika Bocco au Kagere kwani anaamini muda wowote wanaweza kufunga mabao.

“Nasikia raha sana kucheza timu moja na wachezaji wakubwa kama Bocco na Kagere ambao kwa kushirikiana kwetu tunaweza kuwafunga wapinzani muda wowote, na hilo tumekuwa tukilifanya katika mazoezi kwani tunaishi kama familia moja,” anasema Mugalu.

Katika kikosi hicho cha Simba mpaka sasa, Kagere ndiye kinara wa mabao amefunga sita wakati Mugalu amefunga matatu, huko Bocco akiwa amefunga bao moja na jumla yao watatu hao wamefunga mabao manane kati ya 14 ambayo yamefungwa na kikosi kizima mpaka sasa.

LIGI KUU ILIVYO

Kuhusu Ligi Kuu alivyoiona straika huyo, anasema msimu huu itakuwa ngumu kwani kila timu ambayo wamekutana nayo imekuwa ikionyesha ushindani wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa inapata matokeo mazuri dhidi yao. “Sijakaa kuangalia kwa muda mrefu timu baada ya timu, ila ambazo nilipata nafasi ya kuziona zote zimeonyesha ushindani wa kutosha ambao utasababisha ligi kuwa na ushindani wa aina yake, kwani kila mmoja atakuwa na malengo ya kupambana ili kuondoka na pointi tatu,” anasema.

“Uzoefu ambao ninao mara zote hakuna ligi ambayo inakuwa rahisi, lazima uwepo ushindani wa kutosha kutoka kwa kila timu kwani nao watakuwa na malengo ya kufanya vizuri na wengine kutaka ubingwa kama Simba ambavyo tumejiwekea malengo yetu.”