CHILUNDA: Hajakata tamaa kufikia malengo

Monday February 18 2019

 

By ELIYA SOLOMON

KAMA mshambuliaji wa Tottenham Hotspur ya England, Harry Kane angekuwa mshikaji wa Shaaban Idd Chilunda bila shaka angemwambia, usikonde mwanangu nenda kakamue kwa mkopo na kumtolea mifano jinsi alivyosota.

Sio poa kabisa, usione amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Mauricio Pochettino, ukadhani amepitia maisha ya raha kwenye soka lake na kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha Spurs.

Ukiachilia mbali, Kane alianzia soka lake kwenye klabu za Ridgeway Rovers, Arsenal, Ridgeway Rovers na Watford pia ni zao la Tottenham ambako alipita kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza.

Mara baada ya kupandishwa ndio msoto wa kutupwa kwa mkopo ulipoanza kama ilivyo kwa Chilunda ambaye hivi karibuni klabu yake ya CD Tenerife ya Ligi Daraja la Kwanza Hispania, ilivyoamua kumpeleka CD Izarra ya Ligi Daraja la Pili nchini humo.

Kane baada ya kupandishwa Tottenham mwaka2009, hakuwa na nafasi ya kucheza maana tayari kikosi chao hasa kwenye idara yake ya kilikuwa imesheheni watu wa maana.

Kwa kipindi hicho Spurs ilikuwa na vijina wa kazi kama vile, Peter Crouch, Jermain Defoe, Muiceland Eiður Guðjohnsen na Mromania, Roman Pavlyuchenko.

Walichofanya Spurs ni kuamua kumtoa kwa mkopo, 2011 ambapo alijiunga na Leyton Orient, Millwall, Norwich City, Leicester City kote huko alizungushwa kama pia kwa miaka mitatu, alivyorejea alikuwa mtu mwingine.

Uwezo wake wa kufunga uliongezeka mara dufu kutokana na uzoefu alioupata huko alipokuwa akizunguka kwa mikopo, Chilunda anaweza asitofautiane na Kane.

Kilichomfanya mshambuliaji huyo wa Kitanzania kushindwa kufanya vizuri akiwa na CD Tenerife ni changamoto kadhaa ambazo alikuwa akikumbana nazo ikiwemo upya wa mazingira pamoja na lugha.

Kocha wa Tenerife, José Luis Oltra aliwahi kuweka wazi kuwa Chilunda ni mchezaji mzuri lakini changamoto iliyopo mbele yake ni lugha mbayo inamtatiza kwa kiasi kikubwa Hispania wao wanatumia Kihispaniola katika mazungumzo yao ya kawaida.

Hivyo ilikuwa ikimuwia vigumu kuelewa nini ambacho wenzake walikuwa wakielekeza wakati wa mazoezi ndio maana alishindwa kuingia kwenye mifumo ya Mhispania huyo ambaye enzi zake alitamba akiwa na Levante pamoja na Elche za nchini humo.

Akizungumzia maisha yake mapya akiwa na CD Izarra, Chilunda alisema ni mazuri na taratibu ameanza kuzoea maisha ya Hispania ambayo kama mtu huna subira unaweza kurejea nyumbani.

“Kwa sasa kuna baridi kali ambalo linaathiri hadi ngozi yangu, naupenda mpira siwezi kuwa na mawazo ya kurejea nyumbani japo nawakumbuka ndugu na marafiki zangu”

“Natakiwa kuendelea kupambana natambua baada ya muda mfupi kila kitu kitakaa sawa, haikuwa rahisi hata Azam kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza”

“Nilisota kikosi B na baadaye nikaanza kuaminiwa na kupata nafasi ya kucheza, ninafura kuwa hapa kwa mkopo, kikubwa ni kuimarika na nitakaporejea naweza kuwa Chilunda mwingine

“Huu nauchukulia ni mwanzo mpya kwangu nimeshasahau maisha ya Tenerife natizama nini natakiwa kufanya hapa nilipo nikirejea kule ndipo akili na mawazo yangu yatakuwa kwao,” anasema.

CD Izarra ambayo amejiunga nayo kwa mkopo jina lake kamili inaitwa Club Deportivo Izarra, ilianzishwa 1924, inatumia uwanja wa nyumbani wa Merkatondoa, Estella wenye uwezo wa kuingiza watazamaji, 3,500.

Ipo chini ya mwenyekiti, Alfonso Canela, anayekinoa kikosi hicho ni Rodrigo Hernando.

Tangu Chilunda amejiunga na timu hiyo ya Ligi Daraja la Pili amecheza mchezo mmoja ambao walipoteza kwa mabao 2-1 mbele ya Racing Santander.

Chama hilo lipo kwenye hatari ya kushuka daraja hivyo Chilunda anamtihani wa kuipigania timu hiyo kusalia Ligi Daraja la Pili ambayo inaongozwa na Racing Santander wenye pointi 53 huku wao wakiwa na pointi 25 katika nafasi ya 17.

Kama ilivyokuwa kwa Kane basi hata kwa Chilunda inawezekana maana nia na dhamira ya kweli anayo ya kusaka mafanikio kwenye soka la Ulaya.

Advertisement