CHANZO CHA YANGA KUMTIMUA KOCHA NI HIKI

Yanga jana usiku baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Coastal Union na kushinda mabao 3-0 walitoa taarifa ya kusitisha mkataba wa kocha wao Mserbia, Zlatko Krmpotic. Chanzo makini kutoka ndani ya Yanga walilipenyezea habari Mwanaspoti mapema kabla ya taarifa rasmi kutoka kuwa kazi ya kusitishiwa mkataba kwa Zlatko imefanywa kwa ushawishi mkubwa wa mastaa wa timu hiyo waliomkataa.

Inaelezwa tangu mapema mabosi wa Yanga walikuwa hawakubaliani na jinsi ubora wa soka linalopigwa na timu yao, lakini ziara mbili ya mabosi wa juu katika kambi yao iliyopo nje kidogo ya mji wa Kigamboni ikamaliza kila kitu.

Sababu kubwa ya wachezaji kumkataa Zlatko kwa mujibu ya chanzo hicho ni mazoezi duni walikuwa wakipewa na Mserbia huyo.

Inadawai wakati kocha huyo akipambana kuweka mambo sawa, kundi kubwa la wachezaji wamedai wamekuwa wakilazimika kuwa na ratiba ya mazoezi binafsi katika kuwa sawa ndani ya timu hiyo.

Ratiba ya mazoezi machache imewafanya baadhi ya wachezaji kuongezeka uzito na kushindwa kuanza vyema na kuwa katika ubora wa kucheza vyema.

Katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar dalili hizo zilianza kuonekana wazi baada ya Yanga kuonekana wachezaji kukata pumzi ingawa baadaye waliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mapema mabosi wa Yanga walikuwa wanalalamikia chini chini ubora wa soka linalopigwa huku pia washambuliaji nao wakilia na ugumu wa wao kuweza kufunga kutokana na mazingira magumu ya mfumo.

“Hapa tumelazimika kuwa na mazoezi binafsi, wapo ambao wanafanya gym lakini tupo wengine ambao tunafanya uwanjani usiku kwa siri,” alisema mmoja wa mabeki wa timu hiyo.

“Unajua kama unaenda Taifa pale na mazoezi ya kocha huyu unaweza kurushiwa makopo kwa hiyo nikisikia kocha amefukuzwa wala sishangai,” alieleza mmoja wa washambuliaji wa timu hiyo.

SENZO AMALIZA KAZI

Mapema Septemba 29, Senzo Mazingisa ambaye ni bosi wa ushauri wa masuala ya uongozi alimweka kitimoto kocha huyo na wasaidizi wake wote kwa saa saba, kiasi cha kumfanya Zlatko kuchelewa mazoezi ya siku hiyo akitaka kupata maelezo na maendeleo ya kikosi chao.

Ingawa, Senzo hakutaka kueleza undani wa kikao chake na makocha hao alipobanwa na Mwanaspoti, lakini inaelezwa aliwataka kupambana kubadilisha haraka mambo ya ufundi.

Inaelezwa ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Senzo juzi kambini ndio ilitibua mambo.

Inaelezwa Senzo alifanya ziara ya kushtukiza kambini, kisha kupata taarifa ambazo hazikumfurahisha na jana asubuhi akiwa na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said walitimba tena kambini hapo na ndio ikawa mwisho wa ajira ta Zlakto.

Kocha huyo usiku wa jana alikuwa na mchezo dhidi ya Coastal na inaelezwa ndio ulikuwa mchezo wake wa mwisho kabla ya kuanza safari ya kurudi kwake kwani tayari mabosi wa Yanga walishakuwa na mwafaka wa kumwondoa na wakati wowote kuanzia leo watatangaza hatua hiyo baada ya kukubaliana naye kila kitu na kumfanya kocha huyo aitumike Yanga kwa siku 35 tangu atue nchini.

Yanga ilimtangaza Zlatko kuwa kocha wake, Agosti 29 na katika muda wote aliokaa na Yanga ameiongoza timu hiyo kwenye mechi nane, ikiwamo ya jana dhidi ya Coastal na nyingine nne za Ligi Kuu na tatu za kirafiki na zote alipata ushindi dhidi ya Aigle Noir ya Burundi, Mlandege na KMKM.

Katika ligi ukiachana na mechi ya usiku wa jana, alitoka sare ya 1-1 na Tanzania Prisons na kuzichapa Mbeya City, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar kila moja kwa bao 1-0.