CEO mpya Simba aanza na Al Ahly

OFISA Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez ametembelea Makao Mkuu ya klabu ya Al Ahly yaliyopo jijini Cairo, Misri.

Barbara ameongozana na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mulamu Ng'hambi kwa lengo la kukubaliana katika kushirikiana kwenye maeneo ya biashara, ufundi na uendeshaji wa wachezaji.

Kupitia ukurasa wa Instagram wa klabu ya Simba, umeeleza safari hiyo imewafanya viongozi wao kuingia makubaliano ya kushirikiana katika ufundi na uendelezaji wa wachezaji  kwa kujenga kituo cha kukuza vipaji.

"Kwa kushirikiana naAl Ahly kitajengwa kituo nchini ikiwa ni mara ya kwanza  nje ya Misri (barani Afrika) ambacho kitaendeshwa na Simba na klabu hiyo" imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa wamekubaliana hapo baadaye timu hiyo kucheza mchezo wa kirafiki na Simba, mechi itakayochezwa hapa nchini.

Awali Simba walipanga kucheza na Al Ahly wakati wa maadhimisho ya Simba Day lakini ilishindikana kwa wakati huo mipaka ya nchi mbalimbali ilikuwa haijafunguliwa kutokana na uwepo wa janga la virusi vya corona.