CEO Simba afichua ishu ya Senzo

Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba, Barbara Gonzalez ‘Boss Lady’ amesema anajisikia fahari kuiongoza klabu hiyo akiwa na umri mdogo na kufichua siri ya alikomtoa Senzo Mazingisa aliyehamia Yanga.

Barbara (30), alisema alikutana na Senzo mara ya kwanza Afrika Kusini alipotumwa kwenda kumfanyia mahojiano wakati huo klabu inatafuta Ofisa Mtendaji Mkuu.

Alisema jukumu la kufanyia mahojiano Senzo alipewa na bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo baada ya kuanzisha mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu na walimtuma kutokana uwezo wake.

“Nilifunga safari kwenda kukutana na Senzo Afrika Kusini na kumfanyia mahojiano, nilifanya kazi hiyo kwa sababu nina uzoefu mkubwa kwani nimewahi kufanya kazi kampuni ya Deloitte,” alisema Barbara na kusisitiza anachokifanya anakijua na wala habatishi.

“Mimi nipo tofauti na vile watu wanadhani. Nataka zaidi kuona mafanikio wala si maneno. Ni mkali kwenye kazi kwani nataka vitu vifanyike kwa ufanisi na si vinginevyo,” alisema Barbara na kuongeza Simba ni brand kubwa kulinganisha na umri wake, lakini kutokana na uzoefu alioupata katika mashirika mbalimbali unambeba.

“Mimi ni kiongozi, lazima niwe mbunifu katika kazi zangu na kuleta tija Simba, nawaomba niwatoe wasiwasi kuhusu hilo.

Wanachama lazima wajue mimi siyo kocha wala mchezaji, kazi yangu kubwa ni kuona kila idara inafanya kazi yake kwa mahitaji ambayo yataleta ufanisi mkubwa,” alisema.

Kwa mahojiano ya kina zaidi soma kwenye Mwanaspoti kuanzia kesho Alhamisi Septemba 17 pamoja na kurasa zetu za mitandao ya kijamii kama tovuti, Instagram, Facebook na Tweeter.