CAF yakoleza vita ya Yanga, Azam FC

Muktasari:

Tayari Simba na Namungo zina tiketi mkononi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, huku kukiwa na uwezekano wa timu za Tanzania kimataifa kuongezeka kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Dar es Salaam. Uhondo wa Ligi Kuu Bara umehama na sasa ni vita ya Yanga na Azam kusaka nafasi ya pili ili kusikilizia nafasi ya kupata tiketi ya kimataifa zikipambana na timu zinazojinusuru kushuka daraja.

Tayari Simba na Namungo zina tiketi mkononi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, huku kukiwa na uwezekano wa timu za Tanzania kimataifa kuongezeka kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Juzi Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetangaza majina ya timu zitakazoshiriki Ligi ya Mabingwa kwa upande wa nchi zenye nafasi nne na Libya ambayo katika viwango vya CAF ni ya 12 haimo, hivyo kuwepo uwezekano wa Tanzania (ya 13) kuchukua nafasi hiyo.

Kujitoa kwa Ethiopia, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati pia kunaipa nafasi kubwa Tanzania kuongezewa nafasi kwenye ushiriki wa kimataifa kama ilivyokuwa msimu ulipita na iliwakilishwa na Simba, Yanga, Azam na KMC.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao jana alikaririwa na gazeti hili akieleza kusubiri taarifa rasmi ya CAF ili kuona kama Tanzania itaongezewa timu kimataifa na kukiri kusikia taarifa ya Libya kutoshiriki mashindano ya CAF.

Endapo CAF itaipa Tanzania fursa ya kuongeza timu, mchuano utakuwa kati ya Yanga na Azam zinazopambana kusaka nafasi ya pili baada ya Simba kutwaa ubingwa wa ligi.

Yanga yenye pointi 68 inahitaji ushindi leo dhidi ya Mtibwa na Jumamosi dhidi ya Lipuli, ikicheza ugenini ili kujihakikishia nafasi ya pili, hata kama Azam (66) itashinda mechi zote dhidi ya Mbeya City na Prisons.

Kocha Luc Eymael wa Yanga amesisitiza kuitaka nafasi hiyo, baada ya kukosa ubingwa, sanjari na kufungwa na Simba mabao 4-1 kwenye nusu fainali ya FA. “Tutapambana ili kupata nafasi ya pili, tumeukosa ubingwa, tumetolewa pia kwenye FA, hakuna namna zaidi ya kuangalia nafasi ya pili,” alisema.

Kama watafanikiwa kushinda mechi hizo, wataisikilizia CAF katika safari ya kimataifa, huku ikiiweka kwenye nafasi finyu ya kunusurika kutoshuka daraja Mtibwa Sugar ambayo baada ya mechi ya leo itaenda Dodoma kumaliza ligi na Ruvu Shooting.

Ruvu Shooting yenyewe inahitaji sare ili kujinusuru kushuka sawa na Biashara United huku KMC ikihitaji pointi tatu kujinusuru sawa na Prisons na Mbeya City ambayo kesho itacheza na Azam inayohitaji ushindi pia ikiisaka nafasi ya pili.