CAF yaipa TFF Sh 500milioni kuiandaa Taifa Stars kwa Afcon

Muktasari:

  • Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wamesema wataweka hadharani mipango yao Mei Mosi, mwaka huu.

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) itapokea zaidi ya Sh500milioni (dola 260,000) kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ajili ya maandalizi ya timu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon2019) nchini Misri.

TFF itapokea fedha hizo katika mpango wa CAF kusaidia mashirikisho yenye bajeti ndogo ili waweze kuziandaa timu zao vizuri kwa ajili ya fainali hizo za Misri.

Hata hivyo, fedha hizo zitakatwa katika gawio la kila timu wakakazopewa mwisho wa mashindano hayo.

Zawadi kwa bingwa wa mashindano hayo itakuwa ni dola 4.5 milioni na kila timu itakayotolewa katika hatua ya makundi itakuwa na uhakika wa kujipatia dola 475,000.

Iwapo Taifa Stars itafanikiwa kumaliza nafasi ya pili itapokea dola 2.5 milioni, huku kila timu inayofuzu kwa nusu fainali itaondoka kiasi cha dola 2 milioni wakati zile zilizofuzu kwa robo fainali kila moja itapata dola 800,000.

Tanzania iliyo Kundi C pamoja na Senegal, Algeria na Kenya kama itafanikiwa kumaliza nafasi ya tatu itajihakikishia kupata dola 575,000.

Wakati wapinzani wa Tanzania katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), timu za Kenya, Senegal na Algeria zimepanga kuweka kambi Ulaya, Kocha wa Taifa Stars Emmanuel Amunike anatarajiwa kuweka hadharani mikakati yake Mei Mosi, mwaka huu.

Taifa Stars imepangwa Kundi C na Kenya, Algeria, Senegal katika fainali hizo zilizopangwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19, mwaka huu nchini Misri.

Kenya inayonolewa na Kocha Mfaransa Sebastian Migne inatarajiwa kuweka kambi Ufaransa na itacheza mechi mbili dhidi ya Madascar Juni kabla ya kuivaa Uganda Juni 14 au 15. Timu hiyo itaingia kambi Mei 30 hadi Juni 17.

Algeria itaweka kambi Doha na Abu Dhabi itacheza mchezo mmoja wa dhidi ya Mali Juni 16. Senegal itakayoweka kambi Hispania itacheza mechi mbili dhidi ya DR Congo na Nigeria.

Wakati timu hizo tatu zimeanika mikakati yao, Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wamesema wataweka hadharani mipango yao Mei Mosi, mwaka huu.

Amunike alisema anazifuatilia kwa karibu Kenya, Algeria, Senegal na ana taarifa kuhusu maandalizi yao ya kujiandaa na fainali hizo.  

“Tumefuzu Afcon tunajua haya mashindano ni magumu yanatakiwa maandalizi ya mapema, tutacheza michezo ya kirafiki na timu ambazo zimetuzidi ili kujiweka sawa kabla ya fainali,” alisema Amunike.

Hata hivyo, Amunike alisema hawezi kuzitaja timu hizo kwa kuwa bado mazungumzo baina ya nchi hizo yanaendelea. “Ni mapema kusema utacheza na nani kwasababu timu bora Afrika zitakuwa na maandalizi ya kujiandaa kwa fainali hizi, tunazidi kuwasiliana nao kuona ratiba zao ,”alisema Amunike.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema Mei Mosi wataweka hadharani mipango ya maandalizi ya Taifa Stars kuhusu ushiriki wake wa fainali hizo.

"Tumeona wenzetu wameweka wazi mipango yao, sisi Mei Mosi tutatangaza kila kitu ikiwemo wapi tutaweka kambi na timu gani tutacheza nazo mechi za kirafiki,"alisema Kidao.

Wadau

Mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua alisema Amunike anatakiwa kuanza maandalizi mapema ya kujiandaa na fainali hizo.

"Imebaki mwezi mmoja kabla ya kuanza fainali za Afcon, hivyo ni wakati wa kupanga mikakati thabiti kulingana na umuhimu wa mashindano yenyewe,”alisema Chambua.

Nguli huyo alisema kitendo cha kufanya maandalizi ya zimamoto kinaweza kuwa na athari kwa wachezaji kutokana na muda mfupi uliobaki kabla ya kuanza fainali hizo.

Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula alisema huenda TFF imeshindwa kuiweka kambini Taifa Stars mapema kwa kuwa ligi nchini zinaendelea na wachezaji wapo katika kuzipigania klabu zao.

"Kenya, Senegal na Algeria zimetangaza mikakati yao lakini si kwamba zimeanza kambi au mazoezi kwa sababu timu nyingi haziwezi kuanza kambi kwasababu wachezaji wanazitumikia klabu zao naamini muda upo wa kujiandaa na tunaweza kufanya vizuri kwenye Afcon,"alisema Mwaisabula.