CAF yaichongea Simba

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto ameliambia Mwanaspoti kuwa ratiba ambayo itatoka leo haitakuwa na mabadiliko tena na kwamba Simba itabidi wapambane na hali yao kuhakikisha wanamaliza viporo hivyo.

WATANI wa jadi wa soka la Tanzania, Simba na Yanga wote wamelihama jijini asubuhi ya jana kila mmoja akienda mji wake, lakini wakiachana njia panda ya Chalinze, Pwani ili kusaka alama tatu katika mechi za viporo vya Ligi Kuu Bara.

Simba yenyewe iliunganisha barabara ya Segera kuifuata Coastal Union ya Tanga, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, wakati Yanga yenyewe iliunganisha barabara ya Morogoro ikienda mji kasoro bahari kuvaana na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Jamhuri.

Hata hivyo, unaambiwa, mabadiliko ya ratiba mpya wa Ligi Kuu na hasa mechi za viporo vya Simba ni kibarua kizito kwani sasa watalazimika kula viporo vyao kila baada ya siku mbili, hii yote ikitokana na ushiriki wao wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoendeshwa na Chama cha Soka Afrika (CAF).

Yanga inaelekea pale Moro kuifuata Mtibwa huku kocha wao Mwinyi Zahera alishasema kwamba hakuna mechi rahisi kwao kila mchezo ni fainali na wataendelea kutafuta ushindi mechi moja baada ya nyingine na sasa watakutana na wakata miwa hao kesho.

Simba yenye viporo 11 itaanza na Wagosi, lakini Mwanaspoti imepenyezewa taarifa inayoonyesha Wekundu hao watakuwa na kazi nzito katika kuikabili ratiba hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto ameliambia Mwanaspoti kuwa ratiba ambayo itatoka leo haitakuwa na mabadiliko tena na kwamba Simba itabidi wapambane na hali yao kuhakikisha wanamaliza viporo hivyo.

“Ratiba itatoka kesho (leo) tulishaipanga, ni ishu ya kuitoa tu kwa kuwa haitakuwa na mabadiliko kabisa na hatutaki kuona inapanguliwa tena,” alisema Mnguto.

Mnguto alisema ratiba hiyo itawalazimu Simba kila baada ya siku mbili au tatu wacheze mechi moja kwenda nyingine na kwamba sasa hakutakuwa na mabadiliko mpaka viporo hivyo viishe.

“Ratiba itakuwa ngumu kwa Simba kwa kweli watalazimika kucheza mechi moja mpaka nyingine kwa tofauti ya siku mbili au tatu hakuna zaidi, tunachotaka kuona ligi inakwenda vizuri,” alisema.

Alisema ratiba hiyo itaanza rasmi kesho na kwamba ni lazima ligi imalizike kama ilivyopangwa au haraka zaidi kupisha maandalizi mazuri ya kikosi cha Taifa Stars kitakachokuwa kinahitaji muda wa kujiandaa zaidi na Fainali za Mataifa Afrika (Afcon) nchini Misri.

“Tunataka kuona ligi inamalizika kwa haraka au ndani ya wakati tuliopanga, unajua hapo mbele tutahitaji muda wa maandalizi ya kikosi cha Taifa Stars na wachezaji ni hawahawa kwahiyo hili halitakuwa na mabadiliko yoyote.

WASIKIE SIMBA

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema ratiba hiyo licha ya kwamba inawabana, lakini hawana jinsi kwani ligi inahitajika imalizike kwa wakati, watajipanga ili kuona wanaendelea kumaliza salama viporo vyao.

“Ni kweli ratiba imetoka na inatubana kwani kucheza kila baada ya siku mbili ama tatu si kazi nyepesi, lakini hakuna jinsi kwa vile ligi ni lazima imalizike kwa wakati, muhimu ni kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ili kutetea ubingwa wetu.”

Baadhi ya mechi ambazo Simba italazimika kucheza kama viporo ni dhidi ya KMC, Biashara United, Mbeya City, Mtibwa Sugar, Alliance FC, JKT Tanzania, Prisons.