CAF kuiogesha noti Taifa Stars

Muktasari:

  • Ikiwa Stars itafanikiwa kupenya na kuingia hatua ya robo fainali, kiasi cha pesa itakachovuna ni Dola 800,000 (Sh 1.8 bilioni) na kama itaingia nusu fainali itaondoka na kitita cha Dola 1.5 milioni (Sh 3.4 bilioni).

KWA kufuzu tu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Misri mwezi ujao, Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imelihakikishia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupata takribani Shilingi 1 bilioni kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

TFF itapata kiasi hicho cha fedha ikiwa Stars itamaliza ikiwa kwenye nafasi ya nne katika kundi C la mashindano hayo lililo pia na timu za Senegal, Algeria na Kenya lakini kiwango cha fedha kinaweza kuongezeka ikiwa Stars itafanya vizuri na kufika hatua za juu kwenye mashindano hayo.

Kwa mujibu wa mchanganuo wa CAF juu ya fedha za zawadi ambazo hutoa kwa timu kwenye mashindano yake, timu inayomaliza ikiwa nafasi ya nne kwenye kundi la AFCON, inavuna kitita cha Dola 475,000 (Sh 1.09 bilioni) wakati ile inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi inajinyakulia kiasi cha Dola 575,000 (Sh 1.3 bilioni).

Ikiwa Stars itafanikiwa kupenya na kuingia hatua ya robo fainali, kiasi cha pesa itakachovuna ni Dola 800,000 (Sh 1.8 bilioni) na kama itaingia nusu fainali itaondoka na kitita cha Dola 1.5 milioni (Sh 3.4 bilioni).

Bingwa wa mashindano hayo atajinyakulia kiasi cha Dola 4 milioni (Sh 9.2 bilioni) wakati timu itakayomaliza kwenye nafasi ya pili itajiondokea na Dola 2 milioni (Sh 4.6 bilioni).