Bwalya ampa mchongo Wawa

Tuesday March 12 2019

 

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Simba inatakiwa kucheza kwa nidhamu katika safu ya ulinzi ili kupata pointi dhidi ya AS Vita ya DR Congo katika mchezo wa mwisho Ligi ya Mabingwa Afrika, unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba na AS Vita zitamaliza mchezo wao wa mwisho za Kundi D unaotarajiwa kuwa wa kufa au kupona kwa timu zote mbili kwa kuwa kila moja ina nafasi ya kufuzu robo fainali.

Wakati Simba ikitokea katika majeruhi ya kufungwa mabao 2-0 dhidi ya JS Saoura ya Algeria, AS Vita ilishinda bao 1-0 ilipovaana na Al Ahly ya Misri.

Beki nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Frank Kassanga ‘Bwalya’ akizungumzia mchezo huo, alisema safu ya ulinzi imebeba matumaini ya Watanzania.

Kocha Patrick Aussems amekuwa akiwatumia Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa, Juuko Murshid au Paul Bukaba katika safu ya ulinzi.

Alisema haitakuwa na maana kama washambuliaji watafanya kazi nzuri ya kufunga mabao ambayo yatarudishwa na AS Vita kutokana na uzembe wa safu ya ulinzi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Bwalya alisema safu ya ulinzi ya Simba imekuwa ikipoteza umakini hasa wapinzani wao wanapovuka mstari wa katikati kwenda langoni mwao.

Alisema katika mechi tatu ilizocheza Simba nje, safu ya ulinzi ilicheza chini ya kiwango na iliruhusu idadi kubwa ya mabao katika mashindano hayo.

Simba ilifungwa mabao 5-0 na AS Vita, sawa na Al Ahly kabla ya kulala 2-0 na JS Saoura, mchezo uliochezwa Jumamosi usiku.

“Safu ya ulinzi imekuwa ikifanya makosa yaleyale kila mara, hii inaonyesha namna gani hawana nidhamu ya kulinda lango lao. Nimeona mechi zao wamefungwa mabao dhaifu sana walikosa umakini,” alisema Kassanga aliyekuwa akicheza beki wa kati.

Pia alisema Simba haina beki kiongozi ambaye atasimama imara kuongoza safu ya ulinzi na ameshuhudia beki wa kigeni Pascal Wawa akishindwa kwenda na kasi ya mchezo.

Kassanga aliyewahi kucheza Nyota Nyekundu, alisema Wawa na Juuko Murshid wameshindwa kucheza pacha katika nafasi ya beki wa kati ingawa ni mabeki wenye uzoefu na mashindano ya kimataifa. Wawa ni raia wa Ivory Coast na Murshid Uganda.

Nguli huyo alisema hafurahishwi na ukabaji wa mabeki wote wa Simba aliodai wanakaba kwa kufuata kwa nyuma jambo ambalo ni hatari kwa kuwa beki anaweza kusababisha madhara ikiwemo penalti.

“Ukiniuliza beki bora wa Simba nitakwambia Juuko Murshid. Ni mtu anayejituma nashangaa sijui kwanini hatumiki vizuri pale Simba,” aliongeza Kassanga.

Kassanga alisema anaamini safu ya ushambuliaji wa Simba ni nzuri ina uwezo kufunga mabao endapo kutakuwa muunganiko mzuri wa pamoja ndani ya uwanja.

Kauli za wadau

Nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawasa alisema timu hiyo haipaswi kubweteka kwa kuwa inacheza nyumbani.

“Ni mechi ngumu ingawa Simba inaonekana kuimarika siku hadi siku, lazima wachezaji wacheze kwa nidhamu,” alisema Pawasa ambaye ni kocha wa timu ya Taifa ya Ufukweni.

Mchambuzi Ally Mayay alisema Simba inapaswa kumiliki mpira kwa kuwa wapinzani wao wana tabia ya kuanzisha mashambulizi wakiwa katika eneo lao la ulinzi.

Pamoja na kauli za wadau hao, lakini Simba inapaswa kuwa makini na mshambuliaji hatari Jean Marc Mundele ambaye ni hodari wa kufunga kwa kutumia mipira ya adhabu. Idadi kubwa ya mabao ya AS Vita yanatokana na mipira ya krosi au kona.

Advertisement