Buza yaanza kwa kishindo Ligi Kuu Soka la Ufukweni

Muktasari:

Timu hiyo yenye pointi tatu, utofauti wake wa mabao ya kufunga na kufungwa ni 6 ikifuatiwa na Tabata Souls ambayo yenyewe utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa ni 3.

 Ushindi wa mabao 8-2 ambao timu ya Buza imepata dhidi ya Savannah Boys juzi Jumapili, umeifanya timu hiyo ikae kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Soka la Ufukweni iliyoanza Jumamosi iliyopita.

Buza inaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa mbele ya timu za Tabata Souls, Friends Rangers, Six Home City na Friends of Mkwajuni ambazo nazo ziliibuka na ushindi kwenye mechi za raundi ya kwanza zilizochezwa Jumamosi na Jumapili kwenye Uwanja wa Karume jijini.

Timu hiyo yenye pointi tatu, utofauti wake wa mabao ya kufunga na kufungwa ni 6 ikifuatiwa na Tabata Souls ambayo yenyewe utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa ni 3.

Friends Rangers yenyewe ina utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa matatu kama ilivyo kwa Tabata Souls lakini ipo nafasi ya tatu kwa kigezo cha kuwa na idadi ndogo ya mabao ya kufunga kwani wana manne wakati Tabata Souls wana matano.

Nafasi ya nne inashikwa na timu ya Six Home Citu wakati Friends of Mkwajuni yenyewe ipo nafasi ya tano. Mburahati FC iko nafasi ya sita ikiwa na pointi moja na nafasi ya saba inashikiliwa na Kijitonyama Sands Heroes ambayo haina pointi huku Ilala SC ikiwa nafasi ya nane.

Nafasi ya tisa inashikiliwa na timu ya Tanzania Prisons ambayo haina pointi ikifuatiwa na Kisa FC, Vingunguti Kwanza na Savannah Boys ambazo zote hazina pointi.

Michezo ya ligi hiyo itaendelea tena Jumamosi na Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Karume yalipo makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Ligi hiyo inashirikisha jumla ya timu 12 kutoka maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam