Bushoke atwishwa zigo kimataifa

Muktasari:

Bushoke ameliambia Mwanaspoti Online kwamba amefurahia mwaliko huo aliodai unatoa fursa wa kuendeleza Kiswahili kuzungumzwa katika mataifa mbalimbali ya Afrika.

MWIMBAJI wa muziki wa kizazi kipya, Bongofleva,  Bushoke ametwishwa zigo la kuwa kutangaza Kiswahili anga za kimataifa baada ya kuteuliwa kuwa watumbuizaji wa Siku ya Kiswahili na Wanawake 'Swahili Day' itakayofanyika Afrika Kusini Ijumaa ijayo.
Bushoke ameliambia Mwanaspoti Online kwamba amefurahia mwaliko huo aliodai unatoa fursa wa kuendeleza Kiswahili kuzungumzwa katika mataifa mbalimbali ya Afrika.
Amesema tamasha hilo linakutanisha watu mbalimbali kutoka nchini za Afrika, akidai na yeye atakuwa na mchango wake kupitia nyimbo atakazokuwa anaimba kwa Kiswahili.
"Hii ni fursa kwangu kwani tamasha la kwanza lilikuwa la Mandela Day ambalo pia lilikuwa linatambua mchango wa mwasisi wa lugha hiyo, hayati Mwalimu J.K Nyerere, ilikuwa siku ya kipekee kwa kweli kwani niliona namna mataifa mengine yanavyopambana kujua Kiswahili kama lugha muhimu kwao," amesema na kuongeza;
"Awamu hii ni siku ya kinamama yenye lengo la kuhamasisha kuzungumza Kiswahili, nimepewa mwaliko wa kwenda kutumbuiza, hivyo ni nafasi nzuri kwangu kulitumikia taifa kwa njia ya muziki," amesema.
Mwimbaji huyo ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa muziki wa Dansi aliyewahi kutamba na bendi za Bima Lee, OSS na DDC Mlimani Park 'Sikinde', Maximilian Bushoke anafunika na nyimbo zake kadhaa kali ikiwamo Mume Bwege, Dunia Njia, Nalia kwa Furaha, Usiende na nyinginezo zilizompa ujiko mkubwa kwa mashabiki wa muziki nchini.