Burundi yampa kazi ya ziada Ndayiragije

Muktasari:

Taifa Stars iliikaribisha Burundi katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki ulioBurundi kfanyika jana.

Dar es Salaam. Taifa Stars imekubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Burundi katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika jana Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ukiwa moja ya mchezo mgumu na wa kukata na shoka.

Burundi walilazimika kusubiri hadi dakika za mwisho kupata bao pekee la mchezo kupitia kwa Said Ntibazonkiza kwa shuti lililombabatiza beki wa Taifa Stars, Abdallah Kheri na kumshinda kipa David Kisu.

Ulikuwa ni mchezo wa kibabe, ambao ulishuhudia Taifa Stars ikimiliki sehemu kubwa kipindi cha kwanza na kushindwa kutumia nafasi kadhaa walizozitengeneza, hali iliyotokea pia kipindi cha pili.

Kadi mbili za njano alizoonyeshwa kiungo wa Taifa Stars na Simba, Jonas Mkude ilisababisha nafuu kwa Burundi, ambao walionekana kubadilika ghafla na kutumia mwanya huo kuisumbua Taifa Stars.

Ni wazi kuwa kocha Etienne Ndayiragije sasa ana kazi ya ziada kuifundisha timu yake namna ya kumaliza mchezo katika nafasi wanazotengeneza ili kupata matokeo katika michezo ijayo ya kufuzu.

Idd Seleman ‘Nado’, nahodha Mbwana Samatta na Shomari Kapombe wote walikuwa na nafasi nzuri za kuifanya Taifa Stars kuibuka na ushindo mnono kabla ya bao la Ntibazonkiza, lakini utulivu ulishindwa kuwapa faida.

Nado, ambaye alionekana kuwa hatari zaidi kipindi cha kwanza, alikuwa na uwezo wa kuitanguliza Taifa Stars, baada ya pasi safi ya Feisal Salum, lakini shuti lake lilipaa.

Nahodha Samatta alipoteza nafasi nyingine ya kuitanguliza Taifa Stars dakika ya 15, lakini mpira wake wa kichwa ulikosa macho na kwenda nje

Nado alipata nafasi nyingine ya kumjaribu kipa wa Burundi, Onesime Rukundo, ambaye alidaka shuti lake hafifu.

Kipindi cha pili bado kilikuwa bora kwa Taifa Stars, kwani nafasi nzuri aliyopata beki wa kulia, Shomari Kapombe aliishia kushangaza mashabiki, kwani pasi safi ya Said Ndemla alipiga shuti fyongo, ambalo lilishindwa hata kulenga lango

Maumivu zaidi yalikuwa dakika za mwisho, wakati kiungo, Mkude alipoonyeshwa kadi ya pili ya njano kutokana na kusukumana na nahodha wa Burundi, tukio ambalo lilionekana na mwamuzi Martin Saanya.

Awali, Mkude alionyesshwa kadi ya njano kwa tafsiri ya mwamuzi Saanya kuwa aliunawa mpira kwa makusudi wakati Burundi walipokuwa wakishambulia.

Kuanzia hapo, Burundi walionekana kama waliopata nafasi ya kushambulia na kutulia zaidi na kipa wa Taifa Stars, Kisu alianza kuwa katika hatari.

Dakika ya 85 ilileta mabadiliko ya matokeo kwa shuti ambalo lilibadili uelekeo na kumfanya kocha Ndayiragije kumpumzisha Samatta na kumwingiza kiungo Ally Msengi katika kuongeza wingi kati lakini hali haikuwa na mabadiliko yoyote hadi kumalizika kwa mchezo huo.

Mshambuliaji Simon Msuva alisema kupungua kwao uwanjani pamoja na kushindwa kutumia nafasi walizopata kuliwapa nguvu Burundi kurudi mchezoni.

Nahodha wa Burundi, Saido Berahino alisema mchezo ulikuwa tofauti na michezo yote waliyokutana na Tanzania na kuwafanya kuwa makini zaidi muda mwingi wa mchezo wakitengeneza nafasi zao taratibu.