Burkina FC ni mwendo wa vipigo tu Moro

Muktasari:

Timu zilizopokea kipigo kutoka kwa Burkina FC kuwa ni pamoja na timu za 515KJ Ngerengere FC waliocharaza kwa kufunga bao 1-0, Sabasaba United ikatandikwa bao 1-0, Kaizer Chief ikiwabana na kutoa nao suluhu ya 0-0 huku Moro Kids FC wakikumbana na kipigo cha kufungwa bao 4-3.

Morogoro. Timu ya Burkina FC (Kisiki cha mpingo) iliyopo ligi daraja tatu ngazi ya mkoa wa Morogoro 2018/2019 imeendeleza kutoa dozi kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo ili kusaka moja ya nafasi ya kutinga hatua ya michezo ya sita bora katika michezo inayopigwa kwenye dimba la uwanja wa Sabasaba mkoani hapa.
Akizungumza na gazeti hili mjini hapa, Kocha mkuu wa klabu hiyo, Amri Ibrahim alieleza kuwa kwa sasa wanaelekeza akili katika kukinoa kikosi hicho ili kupata nafasi ya kutinga hatua ya sita bora na kutwaa ubigwa wa mkoa huo.
Ibrahim alieleza kuwa kikosi chake kipo vizuri na ari kubwa ya kushinda michezo yote dhidi ya wapinzania wao kwani lengo lao katika ligi hiyo ni kufanya vyema kama sehemu ya maandalizi ya ligi ya mabingwa wa mikoa.
“Burkina FC kwa sasa tunapiga hesabu za kurejea ligi daraja la kwanza kwani tumekuwa tukicheza kwa kujituma, umakini na juhudi lakini tumekuwa tukiwaheshimu pia wapinzani wetu.”alieleza Ibrahim aliyewahi kutamba na kikosi cha Simba SC enzi zake.
Ibrahim alieleza kuwa katika michezo yao minne kati ya mitano ambayo tayari wamecheza wamepata ushindi katika michezo mitatu na sare moja huku wakiwa wamekusanya pointi 10 na kubakiwa na mchezo mmoja wa mwisho dhidi ya Black Viba FC Novemba 23.
Alitaja timu zilizopokea kipigo kutoka kwa Burkina FC kuwa ni pamoja na timu za 515KJ Ngerengere FC waliocharaza kwa kufunga bao 1-0, Sabasaba United ikatandikwa bao 1-0, Kaizer Chief ikiwabana na kutoa nao suluhu ya 0-0 huku Moro Kids FC wakikumbana na kipigo cha kufungwa bao 4-3.
Katibu mkuu msaidizi wa chama cha soka mkoa wa Morogoro (MRFA), Jimmy Lengwe alieleza kuwa ligi daraja la tatu ilianza kutimua vumbi agosti mwaka huu katika vituo vitatu vya Manispaa, Mang’ula na Mvomero ambapo kila kituo itatoa timu mbili.
Lengwe alieleza kuwa timu sita zitawania ubingwa wa mkoa wa Morogoro 2018/2019 na bingwa ndio atayewakilisha mkoa katika ligi ya mabingwa wa mikoa kusaka nafasi ya kutinga ligi daraja pili msimu ujao. MWISHO....