Buguruni wagoma kupiga kura

Saturday December 8 2018

 

By CHARITY JAMES

WANACHAMA wa Yanga tawi la Buguruni wamesema wanaliheshimu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na Serikali hivyo na wao wanaomba waheshimu katiba yao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu tawi hilo, Yassin Yusuph alisema hawapo tayari kushiriki uchaguzi unaosimamiwa na kamati ya uchaguzi ya TFF chini ya mwenyekiti wao, Ally Mchungahela na kuweka wazi kuwa watafute wanachama watakaowapigia kura.
Alisema hawajakataa kufanya uchaguzi na wao wanasubiri tamko kutoka kwa viongozi wao kuhusiana na mchakato wa uchaguzi ili waweze kupata viongozi bora na imara wasiokubali kuyumbishwa na mtu yeyote na watasimamia katiba yao.
"Msimamo wetu ni ule ule hatutapiga kura kuchagua wasaliti ambao wameamua kuchukua fomu kwa matakwa ya TFF na kushindwa kuheshimu katiba yao hasa waliochukua fomu ya kuwania uongozi kwa nafasi ya Mwenyekiti wakati wanajua wazi kuwa mkutano mkuu umepinga uamuzi wa Yusufu Manji kujiuzuru katika nafasi yake," alisema.
"Hatuwezi kuwapigia kura wanafki wanaokiuka katiba ya klabu yao na inavyoonekana TFF inaajenda ya siri kwanini wanang'ang'ania kutuchagulia viongozi wa kutuongoza na hiki kitendo kwa upande wetu tunakiona ni cha ajabu sana kwasababu Shirikisho haliwezi kuingilia na kusimamia majukumu ya mwanachama wake bila ruhusa," alisema.

Advertisement