Bruno, Banega na Lukaku ni vuta nikuvute

ZURICH, USWISI. MAMBO ni moto. Fundi wa mpira, Bruno Fernandes ametajwa kwenye orodha ya wachezaji watatu wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa mikikimikiki ya Europa League.

Wakali wengine watakaochuana na Fernandes kwenye kinyang’anyiro hicho ni kiungo wa Sevilla, Ever Banega na straika wa Inter Milan, Romelu Lukaku.

Fernandes amemaliza michuano hiyo akiwa kinara wa mabao - akifunga mara nane katika mechi 10 alizocheza akiwa na kikosi cha Manchester United na Sporting Lisbon.

Staa huyo wa kimataifa wa Ureno alijiunga na Man United kwenye dirisha la Januari akitokea Sporting Lisbon na tangu atue mambo yake yamekuwa matamu balaa.

Banega alikuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha Sevilla kilichofika fainali na hatimaye kubeba ubingwa huo, wakati Lukaku alikuwa matata kwa kutupia huko Inter - akifunga mabao saba katika

michuano hiyo. Man United iligomea nusu fainali kwa kufungwa na Sevilla wakati michuano hiyo iliporejea kufuatia mlipuko wa corona na mechi ilichezwa moja tu, Sevilla ilishinda 2-1.

Mechi hiyo, Fernandes alifunga kwa mkwaju wa penalti ndani ya dakika 10 za mwanzo, lakini Suso alisawazishia Sevilla na Luuk de Jong akapiga chuma cha ushindi kukifanya kikosi hicho cha kocha Julen Lopetegui kutinga fainali na hatimaye wakabeba ubingwa baada ya kuwachapa Inter Milan.

Kipigo hicho kilimfanya kocha Ole Gunnar Solskjaer amalize msimu bila ya taji licha ya Man United kupewa nafasi kubwa ya kubeba michuano hiyo ya Europa League.

Kabla ya mchezo huo, Fernandes alifunga kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Copenhagen, baada ya mechi hiyo kuingia kwenye dakika za nyongeza.

Kwenye hatua ya makundi, Fernandes alifunga mabao matano, ikiwamo bao maridadi kwenye ushindi wa 4-0 dhidi ya PSV Eindhoven.

Lukaku, kwa upande wake, alifunga bao kwenye fainali kisha akajifunga timu yake ikichapwa 3-2. Ulikuwa mwisho mbaya kwa straika huyo wa zamani wa Man U, ambaye alikuwa na msimu bora chini ya kocha Antonio Conte. Sevilla ilibeba ubingwa, ikiwa ni mara yao ya sita, ikiwa ni nyingi kuliko timu nyingine yoyote kwenye michuano hiyo. Mafanikio ya Sevilla yalitajwa kuchangiwa na Banega, ambaye alikuwa moto kwenye kiungo. Muargentina huyo kwa sasa amehama Hispania na kutimkia Saudi Arabia alikojiunga na Al-Shabab.