VIDEO - Bruce alimtaka Samatta akiwa Wednesday, atamsajili akiwa Newcastle

Muktasari:

Samatta tangu kuanza msimu huu amekuwa akihusishwa kutakiwa na klabu kadhaa za England zikiwemo Newcastle United, Leicester City na West Ham.

Newcastle Upon Tyne, England: Kocha mkuu wa Newcastle United, Steve Bruce aliyewahi kutaka kumsajili Mbwana Samatta akiwa Sheffield Wednesday ameonyesha nia ya kumsajili akiwa Newcastle United.

Kwa mujibu wa jarida la The Chronicle limeripoti kuwa Bruce kwa mara ya kwanza kumtaka mshambuliaji huyo wa Genk ilikuwa alipokuwa na Wednesday.

Newcastler ‘Magpies’ mshambuliaji wake Joelinton aliyesajiliwa mwanzo wa msimu huu amefunga bao moja tu hadi sasa huku Andy Carroll naye akishindwa kuwa msaada kwao tangu aliposajiliw.

Pia, Yoshinori Muto na Dwight Gayle wameshindwa kufikia malengo, jambo linalomfanya Bruce kuanza kuangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji mwingine mwenye uwezo wa kufunga na Samatta anaingia katika rada yake.

BBC Sport iliripoti kuwa Newcastle na West Ham zote zinamtaka Samatta, ambaye alifunga bao dhidi ya Liverpool katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wiki iliyopita na kuongeza thamani yake.

Samatta, 26, ndiye changuo la kwanza kwa Newcastle, na sasa inaaminika kuwa Bruce kwa mara ya kwanza kutaka kumsajili Samatta ilikuwa alipokuwa Sheffield Wednesday mwanzoni mwa mwaka huu alipata taarifa nzuri kutoka kwa marafiki zake.

Wednesday haikufanikiwa kumsajili Samatta, lakini sasa Bruce anaweza kumsajili akiwa Newcastle, kitu pekee kilichokuwa kikwazo kwake kumnasa wakati huo akiwa Wednesday ni timu hiyo kuwa Championship.

Samatta amefunga mabao nane katika mechi 19 alizocheza Genk msimu huu huku akiwa na rekodi yakufunga mabao 32 msimu uliopita, uwezo wake wa kufunga unafunga milango kwake kutua St James' Park.

Endapo Newcastle itafanikiwa kumsajili Samatta atakuwa ni Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu England, na Bruce anataka kuhakikisha anaipata saini ya nyota huyo aliyoshindwa kuipata kabla.

Akizungumzia suala hilo jana baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kwa ajili ya kujiunga na Taifa Stars inayojianda kwa mchezo dhidi ya Equatorial Guinea, Samatta alisema bado hajapokea ofa yoyote ya kwenda kucheza soka la kulipwa England.

"Sijaambiwa lolote na wasimamizi wangu kuhusu ofa ya kwenda Uingereza, hizo naziona tu katika mitandao ya kijamii, lakini sijaambiwa lolote, hivyo siwezi kuzungumza lolote lile" alisema Samatta.

Samatta tangu kuanza msimu huu amekuwa akihusishwa kutakiwa na klabu kadhaa za England zikiwemo Newcastle United, Leicester City na West Ham.