Boxer amkumbuka Zahera

Muktasari:

Boxer amesema licha ya sasa kuwepo Kocha Mbelgiji, Luc Eymael bado ataendelea kumkumbuka Zahera katika maisha yake ya soka.

BEKI wa kulia wa Yanga, Paul Godfrey ‘Boxer’ amemtaja kocha Mwinyi Zahera, akidai kuwa ndiye kocha asiyeweza kumsahau maishani mwake, huku akitangaza kujipanga na vita ya namba na nahodha wake msaidizi, Juma Abdul anayetamba kikosini kwenye namba hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Boxer amesema licha ya sasa kuwepo Kocha Mbelgiji, Luc Eymael bado ataendelea kumkumbuka Zahera katika maisha yake ya soka.

Amesema Zahera licha ya kumpa nafasi ya kutosha wakati akiwa kocha wa Yanga, pia alimsaidia kumbadilisha kutoka winga ya kulia mpaka beki wa pembeni.

“Unajua sikuwa na akili kabisa kama nitakuja kuwa beki wa kulia, lakini Zahera aliniweka chini na kunibadilisha na sasa ni kama nimeshasahau najiona kama nilianza kucheza kama beki tangu zamani,” alisema Boxer.

“Bado napenda kucheza kama winga inategemea na kocha anataka nicheze wapi, kikubwa ninachoshukuru nina kasi hivyo hainipi shida kabisa.”

Hata hivyo, Boxer alisema licha ya kukosa nafasi ya kutosha chini ya Eymael, lakini bado hajakata tamaa katika kukichezea kikosi hicho.

Boxer alisema anajipanga kuhakikisha anapambana kutafuta nafasi kwenye kikosi cha kwanza ambapo, ataendelea kupigania nafasi mbele ya Abdul.

“Sijakata tamaa kutafuta nafasi, najua kuna siku itakuja tu, kitu cha muhimu ni kuwa sawa,” alisema.